Kuendelea uungaji mkono wa kimataifa kwa watu wa Gaza
(last modified Sun, 02 Jun 2024 06:31:28 GMT )
Jun 02, 2024 06:31 UTC
  • Kuendelea uungaji mkono wa kimataifa kwa watu wa Gaza

Wananchi wa maeneo tofauti ya dunia wanaendela kufanya maandamano na mikusanyiko kwa ajili ya kuwaunga mkono wananchi madhulumu na wanaosimama imara wa Ukanda wa Gaza na kusisitiza juu ya kusimamishwa jinai za utawala wa Kizayuni katika ukanda huo.

Waungaji mkono wa wananchi wa Palestina kote duniani wamelaani jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza kwa kufanya maandamano katika miezi ya hivi karibuni.

Wanafunzi wanaoiunga mkono Palestina wamketi kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Santa Cruz katika jimbo la California, Marekani na kutaka kusitishwa uhusiano na makampuni yenye mafungamano na utawala katili wa Kizayuni.
Scott Hernandez Jason naibu chansela wa Chuo Kikuu cha Santa Cruz pia ametangaza kwamba polisi wa Marekani waliwakamata waandamanaji 80 kati yao kwa kushambulia mahema ya waungaji mkono wa Palestina katika uwanja wa chuo kikuu hicho siku ya Ijumaa asubuhi.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Marekani cha Columbia kwa mara nyingine tena wamepinga jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na kutaka kukatwa uhusiano wa chuo hicho na makampuni yanayohusiana na utawala huo wa Kizayuni.

Waungaji mkono wa watu wa Palestina nchini Ufaransa pia wametangaza uungaji mkono wao kwa Wapalestina, hasa katika Ukanda wa Gaza kwa kufanya maandamano katika uwanja wa Jamhuri mjini Paris.

Waungaji mkono wa watu wa Wapalestina

Sambamba na kuongezeka maandamano ya waungaji mkono wa wananchi wa Palestina nchini Ufaransa video nyingi za maafisa wa polisi wanaotumia mabavu dhidi ya raia na waandamanaji zimesambazwa katika mitandao ya kjijamii.

Watetezi na waungaji mkono wa Palestina pia wamefanya maandamano makubwa huko Göttingen, Ujerumani, kupinga jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.

Wakati huo huo, maelfu ya Waislamu wa Bangladesh wameshiriki maandamano ya kuunga mkono Palestina na watu wa Ukanda wa Gaza katika mitaa ya Dhaka, mji mkuu wa nchi hiyo. Huku wakitangaza mshikamano wao na watu wanaodhulumiwa wa Gaza na wamelaani mauaji ya kimbari wanayofanyiwa Wapalestina na utawala katili wa Kizayuni na kudai uhuru wa ardhi ya Palestina.

Waislamu wa Bahrain walijitokeza tena barabarani jioni siku ya Ijumaa iliyopita kwa shabaja ya kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Ukanda wa Gaza na kupiga nara dhidi ya Israel na Marekani. Wamelaani jinai za utawala bandia wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza hususan huko katika mji wa  Rafah kusini mwa ukanda huo.

Wananchi wa Jordan pia wamefanya maandamano ya kuunga mkono Palestina na Ukanda wa Gaza na kutaka kufungwa ubalozi wa Marekani nchini humo kutokana na uungaji mkono wa serikali ya nchi hiyo kwa jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza.

Wakati huo huo waungaji mkono wa Palestina walifanya mgomo wa kuketi chini huko Islamabad mji mkuu wa Pakistan na kupiga nara za kutaka haki ya watu wa Ukanda wa Gaza iheshimiwe na kulaani ukatili wa Israel unaokalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina. Wameitaka serikali ya Pakistani iwasaidie watu wa Palestina hususan wakazi wa Ukanda wa Gaza na kushinikiza vita vya utawala wa Kizayuni visimamishwe mara moja katika ukanda huo.

Ijumaa iliyopita, miji mbalimbali ya Pakistan ukiwemo Islamabad ilishuhudia maandamano makubwa ya kuunga mkono Palestina na Ukanda wa Gaza na kulaani jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina.

Mamia ya waungaji mkono Wapalestina nchini Uingereza waliandamana siku ya Jumamosi katika mji mkuu na miji mingine kadhaa yenye watu wengi kwa wiki ya 33 mfululizo ambapo huku wakilaani jinai za kinyama za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza wametangaza wazi mshikamano wao na watu wa Palestina, watu wasio na ulinzi wala hatia, na kutoa wito wa kusitishwa vita haraka iwezekanavyo. Wamesisitiza kupigwa marufuku kuuziwa silaha utawala wa Kizayuni na kufukuzwa balozi wa utawala huo unaotenda jinai kutoka Uingereza.

Watetezi wa watu wa Palestina pia wamesisitiza kuwa raia wa Uingereza wana misimamo tofauti na serikali yao kuhusu uungaji mkono kwa utawala wa kibaguzi wa Israel na kumtaja waziri mkuu wa nchi hiyo kuwa ni mshiriki katika jinai za utawala huo ghasibu dhidi ya Wapalestina.

Wananchi wa Bosnia pia wamefanya maandamano makubwa ya kuwatetea Wapalestina wanaokandamizwa na kuuawa kinyama na Wazayuni na kusisitiza ulazima wa kusitishwa jinai za kivita zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina hususan katika Ukanda wa Gaza.

Polisi wakiwakandamiza watu wanaotetea Wapalestina

Wananchi wa Morocco kwa mara nyingine wamejitokeza mitaani kutangaza uungaji mkono wao kwa Palestina na watu wa Ukanda wa Gaza na kulaani jinai za utawala bandia wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.

Mjini Tokyo mji mkuu wa Japan, waungaji mkono wa Palestina wamekusanyika mbele ya makao makuu ya Wizara ya ulinzi ya Japan na kutaka kufutwa mkataba wa ununuzi wa ndege zisizo na rubani kutoka utawala dhalimu wa Isael.

Katika mkusanyiko mkubwa mbele ya ubalozi wa Marekani mjini Jakarta, wananchi wa Indonesia wametaka kukomeshwa vita vya utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Kwa muda unaokaribia miezi minane sasa, utawala ghasibu wa Kizayuni huku ukiungwa mkono kikamilifu na Marekani na nchi za Magharibi umefanya mauaji makubwa ya halaiki katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya wananchi wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina, ambapo kwa mujibu wa takwimu za karibuni za Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza, watu elfu 36, 379 wameuawa shahidi na wengine elfu 82, 407 wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo ya kinyama na ya kikatili yanayofanywa na utawala wa Kizayuni tangu tarehe 7, Oktoba mwaka jana.