Jun 18, 2024 10:51 UTC
  • Iran: Tunaichukulia Hija kuwa ni nembo na dhihirisho la umoja na mshikamano

Balozi wa Iran nchini Saudi Arabia amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inaichukulia ibada ya Hija kuwa ni kielelezo na mhimili wa umoja na mshikamano katika safu za Waislamu na ni fursa adhimu ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kufikiria kwa pamoja njia za kutatua masuala ya Waislamu.

Alireza Enayati amesema hayo katika mahojiano na "Independent Arabia" na kuongeza kuwa, mahujaji wa Iran katika Nyumba ya Allah hawafanyi jambo lolote lisilokubaliana na "manasik" na amali za Hija.

Vile vile amesema, mahujaji wanaokaribia 90,000 wa Iran wamepitisha michana na mikesha ya kimaanawi nchini Saudi Arabia kufanya ibada ya Hija kwa utulivu na bila matatizo yoyote huko Makka, na walifanya ziara katika kaburi na msikiti wa Mtume Mtukufu (SAW) na kwenye makaburi ya Baqi kwa utulivu wa hali ya juu.

Alireza Enayati, Balozi wa Iran nchini Saudia

 

Mwanadiplomasia huyo wa Iran ameeleza pia kuwa, mahujaji wa Iran ni miongoni mwa mahujaji wa kawaida katika Nyumba ya Allah na kwamba Jamhuri ya Kiislamu inawaandalia kozi mbalimbali za afya, za kiutamaduni na kidini n.k, kwa ajili ya kuwapa elimu ya kutosha kuhusu Hija, ibada zake na anga yake ya kiroho na kimaanawi.

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Sauda pia amesema kuwa, Taasisi ya Hija ya Iran na Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu umewapanga vyema mahujaji wa Iran, na upande wa Saudia pia kumefanyika juhudi nzuri za kurahisisha masuala ya mahujaji.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, mwaka huu mahujaji wa Iran walikuwa ni 87,550 na walielekea kwenye ardhi za wahyi ndani ya misafara 614 kutoka vituo 21 vya ndege kote nchini Iran. 

Tags