Jun 28, 2024 04:30 UTC
  • Wananchi wa Iran leo wanapiga kura kumchagua mrithi wa  Rais Ebrahim Raisi

Wananchi wa Iran waliotimiza masharti ya kupiga kura leo wanaelekea katika vituo vya kupigia kura ili kumchagua Rais mpya atakayemrithi Ebrahim Raisi aliyekufa shahidi katika ajali ya helikopta Mei 19 mwaka huu.

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa mapema saa mbili asubuhi kwa majira ya hapa Iran huku Tume ya Uchaguzi ikitangaza kuwa, maafisa wake wamejiandaa kikamilifu kuendesha zoezi la uchaguzi huu.

Wairani wasiopungua milioni 61 wametimiza masharti ya kupiga kura. Wagombea wanne wanatarajiwa kuchuana kuwania kiti cha Urais ambao ni Saeed Jalili, mkuu wa zamani wa timu ya mazungumzo ya nyuklia, Muhammad Bagher Qalibaf, spika wa Bunge la Iran, Mostafa Pourmohammadi, waziri wa zamani wa mambo ya ndani na Masoud Pezeshkian, waziri wa zamani wa afya. Wagombea wawili Alireza Zakani, meya wa jiji la Tehran na Amir-Hossein Ghazizadeh Hashemi mkuu wa Wakfu wa Mashahidi na Masuala ya Veterani jana walitangaza kujitoa katika mbio za kuwania urais. Duru mbalimbali zinatabiri kuwa, ushindani mkubwa unatarajiwa kuwa kati ya wagombea watatu ambao ni Saeed Jalili, Muhanmmad Bagher Qalibaf wa mrengo wa wahafidhina na Masoud Pezeshkian wa mrengo wa wapigania mageuzi.

Hadi Tahan Nazif msemaji wa Baraza la Kulinda Katiba ya Iran amesema kuwa, zoezi la upigaji kura litaendelea kwa muda wa masaa 10 kuanzia saa 2 asubuhi mpaka saa 12 jioni na muda huo utaongezwa mpaka mpiga kura wa mwisho aliyeko kituoni atakapopiga kura yake.

Tags