Rais Doumbouya wa Guinea ameapa kutotumia madaraka kwa manufaa yake binafsi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135640-rais_doumbouya_wa_guinea_ameapa_kutotumia_madaraka_kwa_manufaa_yake_binafsi
Rais wa Guinea aliyeapishwa hivi karibuni, Mamady Doumbouya, ameahidi kutotumia vibaya madaraka yake ya urais, akisema ‘‘hatatumia kamwe mamlaka’’ aliyopewa ‘’kwa ajili ya maslahi binafsi’’.
(last modified 2026-01-19T05:43:53+00:00 )
Jan 19, 2026 02:45 UTC
  • Mamadi Doumbouya
    Mamadi Doumbouya

Rais wa Guinea aliyeapishwa hivi karibuni, Mamady Doumbouya, ameahidi kutotumia vibaya madaraka yake ya urais, akisema ‘‘hatatumia kamwe mamlaka’’ aliyopewa ‘’kwa ajili ya maslahi binafsi’’.

Doumbouya aliapishwa rasmi juzi Jumamosi kuwa Rais wa Jamhuri ya Guinea baada ya kuibuka na ushindi wa asilimia 86.72 ya kura katika uchaguzi wa Rais wa Disemba 28 nchini humo na hivyo kuashiria kurejea Guinea katika utawala wa katiba kufuatia kipindi cha mpito cha uongozi wa kijeshi wa zaidi ya miaka minne.

Uchaguzi huo wa Disemba mwaka jana ulikuwa wa kwanza kufanyika nchini humo tangu Doumbouya alipompindua Rais Alpha Conde miaka minne iliyopita.

Jenerali Mamadi Mamady Doumbouya aliapishwa katika hafla iliyofanyika katika uwanja wa Jenerali Lansana Conte huko Nongo, nje kidogo ya mji mkuu Conakry, iliyohudhuriwa na wakuu kadhaa wa nchi za Kiafrika na jumbe za ngazi za juu kutoka pembe mbalimbali duniani. 

Mamady Doumbouya ataiongoza Guinea kwa muhula wa miaka saba. Kwa mujibu wa Kifungu cha 59 cha Katiba ya Guinea, Doumbouya alikula kiapo mbele ya Mahakama ya Juu, iliyoongozwa na rais wake wa kwanza, Fode Bangoura, ambapo amaeahidi kuwa muaminifu kwa taifa hilo na kuheshimu utawala wa sheria.

Rais Paul Kagame wa Rwanda, Bassirou Diomaye Faye wa Senegal, Assimi Goita wa Mali, na Adama Barrow wa Gambia ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria sherehe ya kuapishwa Rais wa Guinea.