Machafuko ya baada ya uchaguzi Cameroon: Waandamanaji wafungwa jela, wengine waachiwa huru
-
Machafuko baada ya uchaguzi wa raisa Cameroon
Mgogoro wa kisiasa unaendelea kuikumba Cameroon wiki chache tu baada ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi kufanya uchaguzi wa rais.
Takriban waandamanaji 30 walizuiliwa usiku kucha kuanzia Ijumaa Desemba 12 hadi Jumamosi Desemba 13 katika Gereza Kuu la Kondengui katika mji mkuu wa Cameroon, Yaoundé.
Wakati huo huo, ofisi ya mwendesha mashtaka wa mahakama ya kijeshi ya Cameroon imewaachia huru waandamanaji wasiopungua 20.
Watu 50 wakiwemo akiwemo mtoto mdogo, waliokuwa wametiwa mbaroni wakati wa maandamano ya baada ya uchaguzi walifikishwa mbele ya mwendesha mashtaka wa mahakama ya kijeshi ya Cameroon. Takriban waandamanaji 30 waliwekwa rumande katika gereza la Kondengui la Yaoundé.
Kundi la mawakili watetezi limetoa wito likitaka kuachiwa huru watu hao wanaotuhumiwa kuhusika na machafuko ya baada ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa mashirika ya kiraia na vyanzo vya serikali, zaidi ya watu 1,000 wamesalia kizuizini kufuatia machafuko ambayo yameitikisa Cameroon baada ya kuibuka hali ya mchafukoge kupinga kuchaguliwa tena Rais Paul Biya.
Mahakama ya Juu ya Cameroon Oktoba 27 ilimtangaza Biya kuwa mshindi wa uchaguzi huo, kwa kupata asilimia 53.66ya kura, akimpita mpinzani wake Issa Tchiroma Bakary, aliyepata asilimia 35.19 ya kura.
Maandamano ya wananchi yalishuhudiwa katika maeneo kadhaa ya Cameroon siku chache baada ya uchaguzi wa raisa wa Oktoba 12 mwaka huu. Issa Tchiroma Bakary kwa upande wake amepinga matokeo ya uchaguzi wa rais na kusema yeye ndiye mshindi wa uchaguzi wa rais wa Cameroon.
Tchiroma amesisitiza kuwa Biya ametunukiwa ushindi wa "udanganyifu" katika uchaguzi huo.