Masoud Pezeshkian ashinda kiti cha urais Iran
Massoud Pezeshkian amechaguliwa kuwa Rais wa 9 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya kupata kura nyingi zaidi za wananchi katika duru ya pili ya uchaguzi uliofanyika jana Ijumaa.
Mashirika mbalimbali ya habari yametangaza habari hiyo na kunukuu taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran ikisema kuwa, Pezeshkian amekuwa Rais mteule wa Iran baada ya kuhesabiwa na kujumlishwa kkura za uchaguzi wa 14 wa Rais. Pezeshkian amepata ushindi huo baada ya kukomba kura 16,384,403. Mpinzani wake Saeed Jalili amepata kura 13,538,179.
Duru ya pili ya uchaguzi wa 14 wa Rais wa Iran ilifanyika Ijumaa ya jana ya Julai 5 ambapo zaidi ya watu 30,530,157 walijitokeza kupiga kura.
Masoud Pezeshkian na Saeed Jalili, wagombea wawili waliopata kura nyingi zaidi katika duru ya kwanza ya uchaguzi iliyofanyika Ijumaa iliyopita, Juni 28, wamegombea kiti cha juu cha mhimili wa utendaji ndani ya mfumo Jamhuri ya Kiislamu yaani Serikali katika uchaguzi wa jana.
Muda wa kupiga kura katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais wa Iran iliyofanyika jana kote nchini Iran, ulirefushwa hadi saa sita usiku kutokana na wananchi kujitokeza kwa mamilioni katika uchaguzi huo.
Shirika la habari la Mehr liliripoti kuwa, Tume ya Uchaguzi nchini Iran, kwa idhini ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Ahmed Vahidi, imerefusha muda wa kupiga kura kama inavyosema Katiba, kutokana na kujitokeza idadi kubwa ya wapiga kura.
Uchaguzi huu wa jana wa Rais ambao umeainisha kiongozi wa Serikali ya Awamu ya 14 ya Jamhuri ya Kiislamu umefanyika baada ya kufa shahidi Rais wa zamani wa Iran, Sayyid Ebrahim Raisi ambaye aliaga dunia Mei 19 mwaka huu katika ajali ya helikopta.