Kiongozi Muadhamu amuidhinisha rasmi Dkt Pezeshkian kuwa Rais wa Iran
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemuidhinisha rasmi Masoud Pezeshkian kuwa Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika hafla iliyohudhuriwa na maafisa wa kitaifa na kijeshi hapa Tehran.
Sherehe ya kuidhinisha kura za wananchi kwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu zimefanyika leo asubuhi katika Husseiniya ya Imam Khomeini (MA) hapa Tehran, kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei kumpasisha Dakta Masoud Pezeshkian kuwa Rais wa 9 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa mujibu wa Kipengee cha 9 cha Sura ya 110 ya Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu.
Ayatullah Khamenei katika dikrii aliyotoa katika sherehe hiyo, ameutaja uchaguzi uliohudhuriwa na wananchi wengi na kupata kura nyingi shakhsiya aliyechaguliwa kuwa ni ishara ya kuimarika upande wa Jamhuri wa utawala wa Kiislamu wa Iran na amesisitiza udharura wa kutekelezwa mpango wa kuimarisha uchumi.
Katika sherehe hiyo pia, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran, Ahmad Vahidi ametoa ripoti kuhusu namna uchaguzi wa 14 wa Rais ulivyofanyika hapa nchini. Kadhalika Dakta Pezeshkian amelihutubia taifa katika hafla hiyo.
Dakta Masoud Pezeshkian mwenye miaka 69, anatazamiwa kula kiapo cha kulitumikia taifa Jumanne ya keshokutwa, Julai 30. Alichaguliwa kuwa Rais wa 9 wa Iran baada ya kuibuka na ushindi wa kura milioni 16.3 kati ya zaidi ya kura milioni 30 zilizopigwa katika duru ya pili ya uchaguzi wa 14 wa Rais wa Iran mnamo Julai 5.
Mpinzani wake Saeed Jalili alipata kura 13.5. Anachukua usukani kuongoza serikali ya awamu ya 14 ya Iran, kufuatia kufa shahidi Rais Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta iliyotokea katika mkoa wa Azerbaijan Mashariki, mnamo Mei 19.
Maelezo kamili ya hotuba za Kiongozi Muadhamu na Dakta Pezeshkian yatakujieni katika matangazo yetu yajayo....