Mfalme Salman atoa mwito wa kuimarishwa uhusiano wa Saudia na Iran
(last modified Fri, 02 Aug 2024 02:43:12 GMT )
Aug 02, 2024 02:43 UTC
  • Mfalme Salman atoa mwito wa kuimarishwa uhusiano wa Saudia na Iran

Mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin Abdulaziz Aal-Saud ametoa wito wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbili kati ya Riyadh na Tehran.

Katika ujumbe wake kwa Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian, Mfalme wa Saudia amesisitiza kuwa Riyadh ina hamu ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Tehran.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, ujumbe huo wa Mfalme Salman uliwasilishwa na Waziri wa Nchi wa Saudia, Mwanamfalme Mansour bin Miteb bin Abdulaziz kwa Rais Pezeshkian jana Alhamisi,

Mwanamfalme Mansour pia alitoa salamu za kheri kwa watu wa Iran kutoka kwa Mfalme Salman na Mwanamfalme Mohammed bin Salman, ambaye ni Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia.

Mfalme wa Saudia ameeleza matumaini ya kuchukuliwa hatua zaidi katika kuendeleza uhusiano wa pande mbili na Iran na kuendelea kwa uratibu na mashauriano kati ya pande hizo mbili, ili kukuza amani na usalama wa kieneo na kimataifa.

Aidha amesema Iran na Saudi Arabia zina nafasi muhimu katika eneo na Ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza kuwa, kuboreshwa uhusiano wa pande mbili ni kwa maslahi ya mataifa haya mawili na eneo zima.

Halikadhalika Mfalme Salman wa Saudi Arabia katika waraka wake huo, ameitakia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mafanikio, izza na ustawi.

Tags