Iran: Tuna haki halali ya kujilinda na kujihami
(last modified Wed, 30 Oct 2024 03:30:55 GMT )
Oct 30, 2024 03:30 UTC
  • Iran: Tuna haki halali ya kujilinda na kujihami

Msemaji wa serikali ya Iran, Fatemeh Mohajerani amesema Jamhuri ya Kiislamu ina haki ya kujilinda na kusisitiza kuwa, nchi hii itatekeleza haki hiyo "halali" kwa "wakati na mahali mwafaka."

Katika kikao na waandishi wa habari hapa mjini Tehran jana Jumanne, Mohajerani amebainisha kuwa, utawala wa Kizayuni katika jaribio la kukwepa kushindwa kwake huko Gaza na Lebanon, ulifanya uvamizi na mashambulizi ya anga dhidi ya ardhi ya Iran kinyume na sheria za kimataifa, na kusababisha kuuawa shahidi wananchi watano wa Iran.

Hata hivyo amesisitiza kuwa, uchokozi huo wa utawala wa Kizayuni haujakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuimarisha umoja wa kitaifa wa wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Amesema, "Utawala wa Kizayuni ulidhani kuwa chokochoko zake zitavunja umoja wa kitaifa wa Iran, lakini kinyume chake, umoja na mshikamano miongoni mwa Wairani umeimarika hata zaidi."

Iran inasisitiza kuwa haifuatilii vita, lakini haitafumbia macho haki yake ya kutoa jibu "linalostahiki na thabiti" kwa kitendo cha hivi karibuni cha uchokozi cha utawala wa Kizayuni wa Israel.

Akijibu swali kuhusu msimamo wa Iran kuhusiana na mshindi wa uchaguzi wa rais wa Marekani Novemba mwaka huu 2024, Mohajerani amebainisha kuwa, uchaguzi huo ni suala la watu wa Marekani, na hakuna tofauti yoyote kwa Iran kwa mmoja wa wagombea wawili atakayechukua madaraka.

 

 

Tags