Araghchi: Baraza la Usalama linapasa kuiwekea vikwazo Israel
(last modified Wed, 30 Oct 2024 03:30:26 GMT )
Oct 30, 2024 03:30 UTC
  • Araghchi: Baraza la Usalama linapasa kuiwekea vikwazo Israel

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina jukumu la kuuwekea vikwazo utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na tabia ya utawala huo kuendelea kushupalia vita na umwagaji damu huko Gaza na Lebanon.

Sayyid Abbas Araghchi alisema hayo jana Jumanne katika mkutano na mabalozi na wasimamizi wa ofisi za kibalozi hapa Tehran na kueleza kuwa, "Kuendelea mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza na hujuma za utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon na Syria, na vile vile chokochoko za kijeshi za utawala huo katika maeneo mengine kunatishia amani na usalama wa dunia.

Araghchi ametaka jamii ya kimataifa ichukue hatua kali dhidi ya utawala wa Kizayuni na kusema kuwa, Baraza la Usalama la UN lina wajibu wa kuchukua hatua dhidi ya utawala wa Kizayuni kwa kuendeleza vita na umwagaji damu huko Gaza na Lebanon; na kuuweka vikwazo vikali utawala huo ghasibu kwa msingi wa Ibara ya Saba ya Hati ya Umoja wa Mataifa.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameendelea kusema kuwa, katika kipindi hiki kigumu na nyeti, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza ulazima wa kufanyika juhudi za pamoja za kidiplomasia ili kusimamisha uchokozi na jinai za utawala wa Kizayuni.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa: Iran inataka wanachama wa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na madhubuti za kukomesha mashambulizi ya mabomu na mauaji ya watu wasio na hatia huko Gaza na Lebanon, na kushughulikia mara moja hali mbaya ya wakimbizi kwa kuwezesha wafikishiwe misaada ya kibinadamu katika maeneo husika.

Tags