Sera ya kuunga mkono Palestina, kipaumbele cha serikali ya 14
(last modified 2024-09-06T12:43:04+00:00 )
Sep 06, 2024 12:43 UTC
  • Sera ya kuunga mkono Palestina, kipaumbele cha serikali ya 14

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuunga mkono muqawama wa wananchi wa Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel ni moja ya vipaumbele vya serikali ya 14 na sehemu muhimu ya nguzo za siasa za nje za Iran.

Katika ujumbe wake kwa 'Kongomano la Mujahidina walio Uhamishoni na Kuenzi Huduma za Hossein Amir Abdullahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya 13, kwa Muqawama', Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesisitiza kuendelea siasa za Tehran za kuunga mkono mapambano ya wananchi wa Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel na kusema siasa hizo za kuunga mkono muqawama na malengo matukufu ya wananchi wa Palestina ni moja ya vipaumbele vya siasa za nje za Iran, ambazo hazibadiliki kwa kubadilika serikali zilizoko madarakani.

Rais Pezeshkian amesema, serikali ya 14 itaendeleza siasa za kuunga mkono kikamilifu mapambano ya wanyonge wote duniani dhidi ya hatua za mataifa ya kibeberu hususan muqawama wa taifa madhulumu la Palestina dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Israel unaofanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wasio na hatia. Pezeshkian ameeleza kuwa, wananchi wa Iran daima wamekuwa wakichukizwa na jinai za utawala wa Kizayuni na kuunga mkono haki za wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina, na kwamba wataendeleza uungaji mkono wao huo kwa nguvu zaidi katika siku zijazo. Moja ya baraka kubwa zaidi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nusu karne iliyopita ni uungaji mkono wake kwa muqawama wa taifa madhulumu la Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Kizayuni, na vile vile mapambano ya wanyonge wote duniani dhidi ya mrengo wa kiburi na utumiaji mabavu ulimwenguni, mapambano ambayo yanaimarika kila siku kutokana na uongozi shupavu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na viongozi wengine wa mfumo wa Kiislamu wa Iran katika vipindi tofauti vya uongozi wao, ambapo serikali ya 14 pia inafuata njia hiyo hiyo kwa busara na nguvu zake zote.

Sisitizo la Rais Pezeshkian la kuendelea kuunga mkono muqawama wa wananchi wa Palestina

Katika muktadha huo viongozi wakuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu kuanza duru mpya ya ukatili na mauaji ya umati ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza mnamo tarehe 7 Oktoba, mauaji ambayo yamepelekea kuuawa na kujeruhiwa Wapalestina wapatao elfu 150, wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara katika vikao na mikutano yao na viongozi wa nchi na taasisi za kimataifa ulazima wa kukomeshwa jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia, kuondoa mzingiro wa kidhalimu dhidi yao na kurudisha amani katika eneo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na jamii ya kimataifa zinafanya juhudi kubwa za kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza, huku utawala huo ukitumia visingizio mbalimbali kukwamisha mazungumzo ya kusitisha vita katika ukanda huo ili kwa njia hiyo uweze kufikia malengo yake haramu ya kisiasa na kijeshi dhidi ya Wapalestina.

Moja ya sababu za kuendelea uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kadhia ya Palestina ni kuhusiana na asili na utambulisho wa mfumo wake wa kisiasa ambapo katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza suala la kuwatetea wanaodhulumiwa duniani dhidi ya madhalimu na mataghuti. Kuhusu suala hilo, Wapalestina ndio watu wanaodhulumiwa zaidi ulimwenguni na ambao wanakabiliwa na jinai za Wazayuni zisizo na mfano wake katika miongo 8 iliyopita. Wazayuni sio tu kwamba wanaikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina kwa uungaji mkono wa nchi za Magharibi, bali pia wanatesa na kuwaua kwa umati Wapalestina kwa uungaji mkono wa Wamagharibi hususan Marekani, suala ambalo limedhihirika wazi katika mauaji ya kimbari ya miezi 11 iliyopita huko Gaza.

Mauaji ya umati na uharibifu wa utawala wa Israel Gaza

Sababu nyingine ya uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa Palestina ni kwamba wananchi wa Palestina wenyewe wamechukua stratijia ya muqawama dhidi ya Wazayuni watenda jinai, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia inaunga mkono muqawama huo wa kupigania uhuru na wa kupigiwa mfano wa Wapalestina. Sababu nyingine ni kwamba muqawama wa Palestina unatokana na mafundisho ya Uislamu, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikiwa ni muungaji mkono wa nchi na mataifa ya Kiislamu, inaona kuwa ni wajibu wake kuunga mkono kadhia ya taifa la Palestina. Katika hali hiyo, hapana shaka kwamba pamoja na mashinikizo na matatizo yote yaliyopo njiani, lakini kipindi hiki kigumu kwa Wapalestina na eneo zima kitapita tu, ambapo kwa kudumishwa azma na kujitolea wananchi wa Palestina sambamba na uungaji mkono wa mhimili wa muqawama, utawala uanotenda jinai wa Israel, kama zilivyokuwa serikali na tawala nyingine dhalimu, zenye kiburi na zilizotumia mabavu katika historia, nao pia hivi karibuni utasalimu amri mbele ya matakwa ya watu wa Palestina, na hatimaye watu hao kupata fursa ya kuunda taifa huru la Palestina, mji mkuu wake ukiwa ni Beitul Muqaddas (Jerusalem).

Tags