Iran yakanusha madai ya Magharibi: Hatujaipatia Russia makombora yoyote ya balestiki
(last modified Sat, 07 Sep 2024 11:53:44 GMT )
Sep 07, 2024 11:53 UTC
  • Iran yakanusha madai ya Magharibi: Hatujaipatia Russia makombora yoyote ya balestiki

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha madai kwamba inaipatia Russia makombora ya balestiki na kusisitiza kuwa madai hayo yanayotolewa na Marekani na washirika wake wa Magharibi ni ya upotoshaji na hayana msingi wowote.

Ofisi ya uwakilishi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imeeleza katika taarifa iliyotoa Ijumaa kwamba Tehran inauchukulia kuwa si ubinadamu usaidizi wowote wa kijeshi unaotolewa kwa pande hasimu katika vita vya Ukraine, usaidizi ambao unaongeza maafa ya roho za watu na uharibifu wa miundombinu nchini Ukraine.
 
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kwa sababu hiyo, sio tu Jamhuri ya Kiislamu haifanyi jambo kama hilo, lakini pia inazotolea mwito nchi zingine kuacha kuzipatia silaha pande zinazohusika katika vita hivyo.
 
Ofisi ya uwakilishi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imesisitiza kwa kusema: msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu mzozo wa Ukraine haujabadilika.
Silaha za Marekani inazopelekewa Ukraine

Sisitizo hilo limetolewa baada ya wajumbe wa Marekani, Uingereza na Ufaransa kutoa shutuma zilizoratibiwa kwa pamoja dhidi ya Tehran kuhusu  mzozo unaoendelea kati ya Russia na Ukraine, wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika Agosti 30.

 
Ofisi ya uwakilishi ya Iran UN imezitolea mwito nchi nyingine, nazo pia kuiga mfano huo na kukomesha upelekaji silaha kwa pande zinazopigana.
 
Awali kabla ya hapo, Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa Amir Saeed Iravani, alikanusha kile alichokiita tuhuma "zisizo na msingi na za upotoshaji" za Marekani, Uingereza na Ufaransa za kuihusisha Tehran katika operesheni za kijeshi za Russia nchini Ukraine.
 
Katika barua aliyomwandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama la umoja huo siku ya Jumatano, Iravani alisema: "Marekani na washirika wake hawawezi kukataa ukweli usiopingika kwamba kutuma silaha za kisasa Magharibi na hasa Marekani, kumerefusha vita nchini Ukraine na kuwadhuru raia na miundombinu ya kiraia."
 
Mwakilishi wa kudumu wa Iran UN alisisitiza katika barua yake hiyo kwamba, Iran "inakanusha kwa msisitizo kamili" madai yoyote ya kuihusisha na uuzaji, usafirishaji au uhamishaji wa silaha kinyume na wajibu ilionao kimataifa kuhusiana na Russia na kuyaelezea madai hayo kuwa ni "upotoshaji usio na msingi wowote."

Tehran imeshakanusha mara kadhaa madai ya Magharibi kwamba inajihusisha na vita kati ya Russia na Ukraine.

Aidha, Iran imekuwa ikitoa mwito wa kusitishwa mapigano na kusisitiza kuwa kuendelea vita nchini Ukraine kunachangiwa zaidi na upelekaji silaha nchini humo unaofanywa na nchi za Magharibi.../