Sep 10, 2024 02:26 UTC
  • Russia: Iran ni waitifaki wetu, lakini si kweli kwamba wametupa makombora

Ikulu ya Kremlin imekanusha vikali madai ya jarida la Wall Street Journal la Marekani lililodai kuwa Iran imeipa Russia makombora ya masafa mafupi ya balestiki ili yatumike katika vita vinavyoendelea nchini Ukraine.

Msemaji wa Ikulu ya Russia ya Kremlin, Dmitry Peskov, alisema jana Jumatatu kwamba ameiona ripoti hiyo kwenye jarida la Marekani la Wall Street Journal, lakini madai na ripoti zote kama hizo si sahihi na hazina ukweli wowote.

Peskov amewaambia waandishi wa habari kwamba: "Iran ni mshirika wetu muhimu, tunaendeleza uhusiano wetu wa kibiashara na kiuchumi, tunaendeleza ushirikiano wetu katika nyanja zote zinazowezekana, pamoja na zile nyeti zaidi, lakini madai kuwa Iran imetupa makombora, hayana ukweli wowote." 

Tarehe 6 mwezi huu wa Septemba jarida hilo la Marekani lilinukuu maafisa wasiojulikana wa Marekani na Ulaya wakidai kuwa eti Iran imeipaa Russia makombora ya masafa mafupi ili yatumike dhidi ya Ukraine.

Jana Jumatatu pia, Umoja wa Ulaya ulirudia madai hayo hayo yasiyo na msingi ukisema taarifa eti Iran imeipa Russia makombora ya masafa mafupi ya balestiki kuisaidia Moscow kupigana vita nchini Ukraine.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan’ani pia jana Jumatatu alikanusha madai hayo na kusisitizia msimamo wa wazi wa Tehran kuhusu vita vya Ukraine akisema: "Inasikitisha kuona kwamba pande zinazochochoa mgogoro na vita huko Ukraine zinajipa uthubutu wa kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran."