Sep 13, 2024 07:32 UTC
  • Amir Saeid Iravani
    Amir Saeid Iravani

Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa mjini New York amepinga vikali madai ya kuwepo majaribio ya kuwamaliza wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu nje ya nchi akiyataja kuwa ni "uzushi" uliobuniwa na maadui.

"Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina nia  wala mpango wowote wa kutekeleza mauaji au utekaji nyara uliopangwa, iwe katika nchi za Magharibi au nchi nyingine yoyote," imesema taarifa ya mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Iravani.

Amesema kuwa, tuhuma na uzushi huo  dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu kupanga kuua wapinzani nje ya nchi umebuniwa na utawala wa Kizayuni wa Israel na kundi la kigaidi la wanafiki, MKO.

Amir Saeid Iravani ameongeza kuwa, "Uzushi huu umetengenezwa na kuenezwa na utawala wa Kizayuni, kundi la kigaidi la MKO lenye makao yake Albania, na idara za ujasusi za baadhi ya nchi za Magharibi - ikiwemo Marekani - ili kupindisha mazingatio ya walimwengu kutoka kwenye ukatili unaofanywa na jeshi la utawala wa Israel huko Gaza."

Kauli hiyo inakuja baada ya Wizara ya Sheria ya Marekani na waendesha mashtaka wa nchi hiyo kudai Jumatano wiki hii kwamba, mwanaume mmoja raia wa Pakistani, amefunguliwa mashtaka kwa tuhuma za kupanga kumuua afisa wa Marekani ili kulipiza kisasi mauaji yaliyofanywa na jeshi la kigaid la nchi hiyo dhidi ya kamanda mkuu wa kupambana na ugaidi, Jenerali Qassem Soleimani, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad mwezi Januari mwaka 2020.

Madai hayo ya Marekani pia yametolewa huku jamii ya kimataifa ikiiandama Israel inayosaidiwa na Washingron, kutokana na kushambulia shule inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa huko Gaza ambako karibu watu 20 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa. 

Tags