Rais wa Iran: Hakuna shetani aliye na ujasiri wa kuishambulia Iran
Rais wa Jamhuri ya Iran amesema kuwa, shetani yeyote hawezi kuthubutu kuivamia kijeshi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokan na nguvu na uwezo wake mkubwa wa kijeshi wa kumzuia adui.
Kwa mujibu wa IRNA, Rais Massoud Pezeshkian wa Iran ameyasema hayo mapema leo katika gwaride la vikosi vya Majeshi ya Iran kwa mnasaba wa Wiki ya Kujihami Kutakatifu mjini Tehran, na kuongeza kwamba dunia nzima ilijaribu kuizuia Iran kuendelea na mapinduzi yake ya Kiislamu, lakini uwepo wa wananchi na majeshi ya nchi kavu, anga na baharini kumewafanya maadui washindwe kuchukua hata kipande cha ardhi ya Iran.
Akigusia kujitosheleza Iran katika sekta ya ulinzi na zana za kijeshi kwa kuwategemea wanasayansi na wasomi wa ndani ya nchi, Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inautangazia ulimwengu kwamba pamoja na uwezo wake wa kujilinda, umoja na mshikamano kati ya nchi za Kiislamu, ni jambo ambalo linaweza kuhakikishia eneo amani, usalama na utulivu. Aidha amesema umoja huo pia unaweza kuuzuia utawala wa Israel ambao ni utawala ghasibu, mfyonza damu, mtekeleza mauaji ya kimbari na mtenda jinai kundeleza jinai hizo katika eneo.
Ikumbukwe Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, majeshi ya dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein yalianza kufanya mashambulio makubwa ya anga na nchi kavu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo vita vya miaka minane vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran vikawa vimeanza. Saddam alidhani kuwa vita hivyo vingedumu kwa wiki moja tu baada ya kutekwa mji wa Tehran. Jeshi la Iraq lilikuwa limefanya uvamizi na mashambulizi kadhaa katika maeneo ya mpakani ya Iran miezi kadhaa nyuma. Magari ya deraya na vikosi 12 vya jeshi la nchi kavu la Iraq viliyashambulia maeneo ya mipaka ya kusini magharibi mwa Iran. Mapambano makali ya wananchi wa Iran yaliwalazimisha askari wa Saddam kurejea nyuma hadi kwenye mipaka inayotambulika kimataifa. Vita hivyo viliendelea kwa miaka minane. Kipindi cha kuanza vita hivyo nchini Iran hujulikana kama Wiki ya Kujihami Kutakatifu.
Mapembano hayo ya kihamasa ya Iran yaliwezesha taifa la Iran kuvuka kwa mafanikio njama zilizokuwa zimewekwa dhidi yake.