Spika wa Bunge la Iran: Zama za uonevu wa Marekani zimekwisha
-
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, ameikosoa Marekani kwa kukiuka Mkataba wa Maelewano kati ya Iran na Marekani (MoU), akisisitiza kwamba "zama za uonevu na ulaghai" wa Washington zimekwisha.
Akizungumzia ukiukaji wa makubaliano hayo unaohusisha Lango-Bahari la Hormuz, kurejeshwa vikwazo vya mafuta dhidi ya Iran, mashambulizi kusini mwa nchi na kuendelea uvamizi wa jeshi la Israel nchini Lebanon, Qalibaf amesisitiza kwamba uhalifu unaofanywa na Washington hautadhoofisha azma ya Iran.
"Ukiukaji mkubwa wa Hati ya Maelewano (MoU) unaofanywa na Marekani unahusu: Kukiuka mamlaka ya Iran ya kusimamia masuala ya Lango Bahari la Hormuz, kurejesha vikwazo vya mafuta, mashambulizi kusini mwa Iran, kuendelea uchokozi wa Wazayuni dhidi ya Lebanon," Spika wa Bunge la Iran amesema kwenye mtandao wa X.
"Enzi ya uonevu na ulaghai imekwisha, hautafika popote, sisi si watu wa kurudi nyuma au kupiga magoti," amesema Spika Qalibaf akimwambia Donald Trump.
Mnamo Julai 17, Iran na Marekani zilisaini Mkataba wa Maelewano (MoU) uliosimamiwa na Pakistan, ambao unatoa wito wa kukomeshwa uhasama daima katika pande zote na unajumuisha ahadi ya kufanya mazungumzo zaidi kuhusu makubaliano ya mwisho katika kipindi cha siku 60.
Matamshi ya Qalibaf yametolewa baada ya Marekani kushambulia maeneo kadhaa kusini mwa Mkoa wa Hormozgan nchini Iran.
Wakati huo huo Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza rasmi kuwa, katika hatua ya kwanza ya kujibu uchokozi huo wa Marekani, vikosi vya wanamaji na anga vya Jeshi hilo, katika operesheni ya pamoja ya makombora na ndege zisizo na rubani (drones), vimetekeleza kwa mafanikio mashambulizi makali dhidi ya shabaha 85 muhimu za kijeshi za Marekani na kutungua ndege moja ya kisasa ya ujasusi ya adui aina ya MQ9.