Spika wa Bunge asema: Zama za kuitishia Iran bila gharama zimeisha
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i138884-spika_wa_bunge_asema_zama_za_kuitishia_iran_bila_gharama_zimeisha
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Baqer Qalibaf amesema Iran si tena shabaha ya vitisho rahisi vya maadui, akiongeza kuwa uzoefu wa vita viwili vya Marekani na Israel umeonyesha kwamba Iran ina uwezo wa kutoa majibu makali kwa uchokozi wa aina yoyote.
(last modified 2026-06-04T11:27:26+00:00 )
Jun 04, 2026 11:24 UTC
  • Muhammad Baqir Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran( Bunge)
    Muhammad Baqir Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran( Bunge)

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Baqer Qalibaf amesema Iran si tena shabaha ya vitisho rahisi vya maadui, akiongeza kuwa uzoefu wa vita viwili vya Marekani na Israel umeonyesha kwamba Iran ina uwezo wa kutoa majibu makali kwa uchokozi wa aina yoyote.

Katika ujumbe wake kuhusu kumbukumbu ya kuaga dunia mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, Hayati Imam Ruhullah Khomeini, jana Jumatano, Qalibaf alisema enzi ya kutishia Iran bila kubeba gharama za matokeo yake imepita na kuyoyoma.

Spika wa Bunge la Iran amesema katika ujumbe huo kwamba, kwa kuongozwa na mafundisho ya Imam Khomeini, taifa la Iran limeonyesha, katika makabiliano yake ya hivi karibuni na Marekani na utawala wa Israel, kwamba halitakubali kamwe mashinikizo.

"Imam Khomeini alilifundisha taifa la Iran kutosalimu amri mbele ya uonevu... Uchokozi wa aina yoyote utakabiliwa na majibu makali, majuto na na yanayostahiki," amesema Spika Mohammad Baqir Qalibaf.

Qalibaf pia amemtaja na kumuenzi Kiongozi Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei aliyeuawa katika siku ya kwanza ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, ambaye alikuwa akitoa hotuba muhimu katika kaburi la Imam Khomeini kila mwaka kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuaga dunia mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu.

"Kwa damu yake safi, Shahidi Khamenei alihakikisha mwendelezo na dhamana ya harakati ya Imam Khomeini, na akainua juu bendera ya heshima, uhuru na Muqawama kuliko hapo awali, na kisha akaikabidhi kwa vizazi vijavyo," Qalibaf amesema.

Amesema mamilioni ya Wairani, wakiongozwa na mafundisho na urithi wa Imam Khomeini na Ayatullah Khamenei, wataendelea kupinga uingiliaji kati wa wageni kwa lengo la kudhoofisha uhuru wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.