Iran kurusha satelaiti 7 mpya katika anga za mbali
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i116702-iran_kurusha_satelaiti_7_mpya_katika_anga_za_mbali
Mkuu wa Shirika la Anga za Mbali la Iran (ISA) amesema Jamhuri ya Kiislamu inapanga kutuma katika anga za mbali satelaiti tano hadi saba zilizotengenezwa ndani ya  nchi. Operesheni hizo zitatekelezwa kabla ya kumalizika mwaka wa sasa wa kalenda ya Iran unaoishia tarehe 20 Machi 2025.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Sep 23, 2024 22:49 UTC
  • Iran kurusha satelaiti 7 mpya katika anga za mbali

Mkuu wa Shirika la Anga za Mbali la Iran (ISA) amesema Jamhuri ya Kiislamu inapanga kutuma katika anga za mbali satelaiti tano hadi saba zilizotengenezwa ndani ya  nchi. Operesheni hizo zitatekelezwa kabla ya kumalizika mwaka wa sasa wa kalenda ya Iran unaoishia tarehe 20 Machi 2025.

Hassan Salariyeh alisema Jumatatu kwamba shirika lake linalenga kurusha setilaiti kadhaa katika kipindi cha miezi michache ijayo na kuongeza kuwa kazi hiyo inafanyika kwa ushirikiano wa Kikosi cha Anga za Juu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC), Wizara ya Ulinzi, Shirika la Viwanda vya Aanga za Juu (AIO) kwa ushirikiano na mashirika kadhaa ya kigeni.

Salariyeh amebainisha kuwa satelaiti zilizoundwa kikamilifu nchini Iran za Tolo-3 na Zafar-2 zitatumwa kwenye obiti katika miezi ijayo kwa kushirikiana na mashirika ya kigeni.

Mnamo Septemba 14, Iran ilifanikiwa kutuma katika anga za mbali satelaiti ya utafiti ya Chamran 1 iliyotengenezwa nchini ikiwa ni hatua nyingine ya kuvutia katika mpango wa anga za juu wa nchi.

Satelaiti hiyo iliwekwa kwenye obiti kwenye mwinuko wa kilomita 550 juu ya uso wa dunia kwa kutumia roketi la kurusha satalaiti la Qaim- 100. Saa kadhaa baada ya kurushwa katika anga za mbali, satelaiti hiyo ya utafiti ya Iran ilituma taarifa zake za kwanza.

Satelaiti ya Chamran-1 imeundwa na kutengenezwa na wahandisi wa Iran katika kitengo cha anga za juu cha Shirika la Viwanda vya Kieletroniki vya Iran (SAIran), ambalo ni shirika tanzu la Wizara ya Ulinzi ya Iran, kwa kushirikiana na wataalamu wa Taasisi ya Utafiti wa Anga (ARI) na makampuni binafsi nchini Iran.