Rais wa Iran: Nchi za Kiislamu zikate uhusiano wa kiuchumi na Israel
-
Pezeshkian na Miqat
Rais wa Iran amesema, kama nchi za Kiislamu zitakata uhusiano wa kiuchumi na utawala wa Israel unaotekeleza mauaji ya kimbari, utawala huo unaouwa watoto hautaweza tena kutenda jinai na uvamizi.
Mwishoni mwa safari yake huko New York, Rais Masoud Pezeshkian wa Iran alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Lebanon, Najib Miqati na akasema: Utawalal wa Kizayuni wa Israel haujaacha kufanya chochote katika kukanyaga haki za binadamu, sheria na kanuni za kimataifa kufuatia jinai zake dhidi ya binadamu zinazofanyika kwa kuungwa mkono na Marekani.
Rais wa Iran amekosoa vikali misaada ya kisiasa, kifedha na silaha ya Marekani kwa Israel ili kutenda jinai Asia Magharibi na kuongeza kuwa, kwa hakika, kama isingekuwa msaada wa Marekani, utawala huu haungekuwa na nguvu na uthubutu wa kutekeleza vitendo hivyo vya uhalifu.
Pezeshkian amekumbusha majukumu ya nchi za Kiislamu katika kuwaunga mkono na kuwasaidia wananchi madhulumu wa Lebanon na Gaza na kufanya juhudi za kukomesha jinai za Israel katika eneo hilo na kuashiria juhudi na mashauriano aliyofanya na wakuu wa nchi za Kislamu zikiwemo Pakistan na Uturuki na pia baadhi ya nchi za Ulaya ikiwemo Ufaransa kwa madhumuni ya kuilazimisha Israel isitishe mashambulizi dhidi ya Lebanon na Gaza. Amesema: Iran iko tayari kuipatia Lebanon msaada wa aina yoyote ile.
Kwa upande wake, Najib Miqati Waziri Mkuu wa Lebanon ameeleza kuwa kile kinachojiri sasa huko Gaza na Lebanon ni kinapingana na ubinadamu na sheria zote za kimataifa. Miqati ameshiria hali ngumu sana wanayopitia wananchi wa Lebanon baada ya hujuma za hivi karibuni za utawala wa Kizayuni na akasema, kutumia vifaa vya kiraia kwa ajili ya kutekeleza mauaji ya raia wa kawaida wasio na hatia ni jinai ambayo inafanywa na utawala wa Kizayuni pekee.
Waziri Mkuu wa Lebanon ameashiria namna Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilivyo bega kwa bega na Lebanon si tu leo hii bali kwa makumi ya miaka sasa na amezitaka nchi nyingine za Kiislamu kuwa na nafasi kubwa katika kuzuia moto wa vita katika eneo la Magharibi mwa Asia.