Iran yakosoa vitendo vya kigaidi vya Israel nchini Lebanon
(last modified Fri, 25 Oct 2024 06:53:18 GMT )
Oct 25, 2024 06:53 UTC
  • Iran yakosoa vitendo vya kigaidi vya Israel nchini Lebanon

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amelaani vikali mashambulizi ya kigaidi ya Israel dhidi ya raia wa Iran mjini Beirut na kuyataja kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na mamlaka ya kujitawala ya Lebanon.

Amir Saeid Iravani alitoa tamko hilo Alhamisi katika barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na rais wa Baraza la Usalama.

Barua hiyo ilifuatia mauaji yaliyotokelezwa kwa makusudi na Israel huko Beirut na kupelekea kuuawa Muirani aliyekuwa na watoto watano na pia daktari wa Iran huko Beirut.

Iravani ameandika kwamba: “Tarehe 19 Oktoba 2024, ndege isiyo na rubani ya Israel ilivurumisha kombora kwenye gari la kibinafsi la raia wa Iran, Bi Masoumeh Karbasi, na mume wake  raia wa Lebanon, katika eneo lenye watu wengi la Jounieh, Beirut. Baada ya kunusurika kwenye shambulizi la kwanza, walitafuta hifadhi kando ya barabara, lakini wakapigwa na kombora la pili muda mfupi baadaye, na wakapoteza maisha.

Ameongeza kuwa katika jinai nyingine mbaya zaidi, mnamo tarehe 22 Oktoba 2024, katika shambulizi la kuchukiza na la makusudi, Israel ilimuua Dakta Ali Heidari, daktari wa Iran na mfanyakazi wa kutoa misaada, huko Beirut. Daktari Heidari alikuwa akifanya kazi za kuokoa maisha, kutoa huduma muhimu za matibabu kwa waliojeruhiwa na kusaidia wale walio na uhitaji mkubwa.

Shahidi Bi Masoumeh Karbasi

Iravani ameyataja mauaji hayo kuwa ni vitendo vya ukatili na ugaidi vinavyofanywa na utawala haramu wa Israel.

Amesema mashambulizi hayo pia yanafichua kutojali kwa Israel kuhusu maisha ya raia na kanuni za kisheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mikataba ya Geneva ya 1949.

Mwandiplomasia huyo wa Iran amelihimiza Baraza la Usalama kulaani mashambulizi ya kigaidi ya Israel dhidi ya raia wa Iran. Aidha  amesisitiza kuwa utawala huo lazima uwajibishwe kikamilifu kwa ukiukaji wake unaoendelea wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.