Tehran: Tuna haki halali ya kujihami mkabala wa uvamizi wa Wazayuni
(last modified Sat, 26 Oct 2024 10:52:48 GMT )
Oct 26, 2024 10:52 UTC
  • Tehran: Tuna haki halali ya kujihami mkabala wa uvamizi wa Wazayuni

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali hatua ya kichokozi ya utawala wa Kizayuni ya kushambulia baadhi ya vituo vya kijeshi hapa nchini, na kuitaja kuwa ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Katika taarifa iliyotolewa leo Jumamosi, wizara hiyo inasisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikitumia haki yake ya asili ya kujilinda kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 51 ya Hati ya Umoja wa Mataifa, inaamini kuwa ina haki na inawajibika kujibu vitendo vya kichokozi kutoka nje ya nchi.

Serikali ya Iran imesisitiza dhamira yake ya kutumia nyenzo zote zilizopo na 'rasilimali za kiroho' ili kulinda usalama na maslahi yake muhimu. Pia imesisitiza wajibu wa pamoja wa nchi zote za kieneo kudumisha amani na utulivu, ikitoa shukrani kwa mataifa ya eneo ambayo yamelaani uchokozi vya Israel.

Kadhalika taarifa hiyo imebainisha kuwa, uvamizi na nyendo haramu za utawala ghasibu wa Israel, yakiwemo mauaji ya kimbari ya watu wa Palestina na uvamizi dhidi ya Lebanon, zikichochewa na uungaji mkono wa kina wa kijeshi na kisiasa wa Marekani na baadhi ya mataifa ya Magharibi, ndiyo vyanzo vikuu vya mivutano na ukosefu wa usalama katika eneo hili.

Mfumo wa kutungulia makombora wa Iran

Iran imezitaka nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa, hususan zile zilizosaini "Mkataba wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari" na "Makubaliano ya Geneva ya 1949," kuchukua hatua za haraka na za pamoja dhidi ya ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesisitiza ulazima wa kuja pamoja jamii ya kimataifa ili kukomesha mauaji ya halaiki, vita na uchokozi huko Gaza na Lebanon na kuzuia vitendo vya kuchochea vita vya utawala ghasibu wa Israel.

Tags