Iran yaanza kuingiza gesi kwenye mashinepewa mpya baada ya azimio la IAEA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i119430-iran_yaanza_kuingiza_gesi_kwenye_mashinepewa_mpya_baada_ya_azimio_la_iaea
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema Iran imeanza kuingiza gesi ya urani kwenye mashinepewa au sentrifuji  za kisasa kama jibu kwa azimio la hivi karibuni la Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA).
(last modified 2024-11-27T23:29:59+00:00 )
Nov 27, 2024 23:29 UTC
  • Iran yaanza kuingiza gesi kwenye mashinepewa mpya baada ya azimio la IAEA

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema Iran imeanza kuingiza gesi ya urani kwenye mashinepewa au sentrifuji  za kisasa kama jibu kwa azimio la hivi karibuni la Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA).

Mohammad Eslami ameyasema hayo mbele ya waandishi wa habari Jumatano jijini Tehran baada ya kikao cha baraza la mawaziri na kuongeza kuwa: "Mpango wa amani wa nyuklia wa Iran uko wazi na chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA)."

Eslami ameonya kwamba shutuma zozote dhidi ya Tehran zitarudisha nyuma ushirikiano uliokuwepo baina ya Iran na IAEA.

Aidha, amekumbusha kuwa mpango wa nyuklia wa Iran uko chini ya usimamizi wa IAEA na kwa kuzingatia Makubaliano ya Kuzuia Uenezaji Silaha za Nyuklia (NPT).

Mkuu huyo wa Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema baadhi ya tuhuma dhidi ya Iran ni za miaka 20 nyuma na zilitolewa kwa ushirikiano wa makundi na taasisi zinazoipinga Iran ili kuzidisha mashinikizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu lakini baadaye zilithibitishwa kuwa hazina ukweli na ni uzushi.

Wiki iliyopita Nchi tatu za Ulaya ziliwasilisha mswada wa azimio kwa Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) zikiituhumu Iran kuwa haiweki wazi shughuli zake za nyuklia.

Itakumbukwa kuwa tarehe 21 Novemba azimio lililopendekezwa na nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani pamoja na Marekani dhidi ya mpango wa amani wa nyuklia wa Iran liliidhinishwa na Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.