Sisitizo la Kiongozi Muadhamu la kuongezwa uwezo wa kijeshi wa nchi
Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Iran amesema, kuongeza utayari na uwezo wa kivita ndilo jukumu muhimu zaidi la vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran alisema hayo Jumatano ya jana 27 Novemba alipokutana na maafisa na makamanda wa Jeshi la Wanamaji la Iran, ambapo sambamba na kuienzi kumbukumbu ya Novemba 28, 1980 ya maadhimisho ya hamasa iliyoonyeshwa siku hiyo na manowari ya Peikan katika kukabiliana na adui wa Kibaathi, na kupelekea kuitwa Siku ya Jeshi la Wanamaji, amesisitiza kuwa jeshi la Wanamaji lina umuhimu mkubwa na mchango wa kipekee katika dunia ya leo.
Matamshi ya Kiongozi wa Mapinduzi katika kikao na makamanda wa jeshi la wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yana nukta kadhaa muhimu za kiulinzi.
Mosi ni kwamba, amesisitiza haja ya kuongeza nguvu za kivita za nchi na kusema kwamba, mwelekeo wa vikosi vya kijeshi, haswa jeshi la wanamaji, katika shughuli zote na mipango inapaswa kulenga kuongeza utayari na nguvu ya kupambana.
Kuongeza nguvu za kivita, au kwa maneno mengine kuangalia mambo kwa uhalisia wake katika mahusiano ya kimataifa ni mojawapo ya hatua muhimu zaidi ambazo serikali lazima zichukue, kwa sababu serikali zinakabiliwa na vitisho vingi kutoka kwa wapinzani na maadui, na kuongeza nguvu za kijeshi kunaweza kupunguza vitisho hivi na kuleta usalama.

Kipengele kingine cha umuhimu wa hotuba ya Amiri Jeshi Mkuu ni kwamba, kazi muhimu zaidi ya jeshi ni kuzuia uvamizi wa maadui. Kwa sura maalumu zaidi ni kwamba, kazi muhimu zaidi ya vikosi vya kijeshi katika nchi yoyote ni kuzuia vita na kuzuia hujuma na uvamizi dhidi ya nchi. Ili kuhakikisha usalama, hatua ya kwanza ni kuongeza nguvu za kijeshi na kuongeza nguvu za kivita.
Kuhusiana na hilo, Ayatullah Ali Khamenei amesema: Uwezo wa kivita kutawezesha kuzuia hujuma za adui na akaongeza kuwa: "kazi muhimu zaidi ya vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ni kuzuia uvamizi, kwa hivyo inapasa muufanye utendaji na uwezo wa kivita wa nchi uonekane mkubwa mbele ya macho ya wanaoitakia mabaya Iran ili wahisi kwa maana halisi kwamba makabiliano yoyote yatakayotokea yatawasababishia hasara na gharama kubwa"
Ukweli wa mambo ni kuwa, matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu juu ya ulazima wa kuongezwa nguvu na uwezo wa kivita yamesimama juu ya msingi wa mantiki ya kuangalia mambo kwa uhalisia wake.

Kipengee cha tatu cha matamshi ya Imam Khamenei ni kuhusu ulazima wa kuendelea na safari za nje ya nchi za Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika miaka ya hivi karibuni, Jeshi la Wanamaji limefanya misheni muhimu nje ya nchi ambapo muhimu zaidi ni Msafara wa 86 wa Manowari za Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Misheni za nje za Jeshi la Jeshi la Wanamaji zinafikisha ujumbe wa nguvu na amani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa nchi za eneo na kwa nchi za dunia.
Wakati huo huo, hatua hiyo inaonesha kuwa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran likiwa na vikosi na wataalamu wa ndani, limefanikiwa kupata mafanikio muhimu sambamba na kuvuka vikwazo vya kidhalimu vya nchi za Magharibi.
Kwa kuzingatia hayo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu anaona kuwa, kuendelea kwa safari za baharini kuwa ni jambo la lazima na akasema: Kama ilivyosemwa hapo awali, ujumbe wa miezi mingi wa Msafara wa 86 wa Manowari za Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na maelezo yake kwa undani yanaweza kuwasilishwa kwa umma kupitia ulimi na tasnia ya sanaa.