Kiongozi Muadhamu awataka Wairani kuwakatisha tamaa maadui Bahman 22
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136440-kiongozi_muadhamu_awataka_wairani_kuwakatisha_tamaa_maadui_bahman_22
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametoa wito kwa taifa la Iran kuonyesha irada, azma thabiti na kusimama kidete, kwa kushiriki kwa wingi katika matembezi na mijumuiko ya kuadhimisha miaka 47 ya Mapinduzi ya Kiislamu, akisema kuwa umoja huo utamkatisha tamaa adui wa nchi hii.
(last modified 2026-02-10T02:29:05+00:00 )
Feb 09, 2026 10:50 UTC
  • Kiongozi Muadhamu awataka Wairani kuwakatisha tamaa maadui Bahman 22

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametoa wito kwa taifa la Iran kuonyesha irada, azma thabiti na kusimama kidete, kwa kushiriki kwa wingi katika matembezi na mijumuiko ya kuadhimisha miaka 47 ya Mapinduzi ya Kiislamu, akisema kuwa umoja huo utamkatisha tamaa adui wa nchi hii.

Katika ujumbe wake kwa taifa la Iran uliorushwa kupitia televisheni kabla ya maandamano ya Bahman 22 (Februari 11) kuadhimisha miaka 47 ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei ameielezea siku hiyo kama dhihirisho la nguvu na hadhi ya taifa la Iran.

"Bahman 22 (Februari 11) kila mwaka ni siku ya kufichua nguvu na hadhi ya taifa la Iran," Kiongozi Muadhamu amesema, akielezea taifa hili kuwa na ari, msimamo thabiti, istiqama, shukurivu, na lenye ufahamu wa hali yake.

Amesema wananchi wa Iran walipata "ushindi mkubwa" mnamo Bahman 22 (Februari 11) mwaka 1979, kwa kujikomboa wenyewe na nchi yao kutoka kwenye minyororo ya "uingiliaji wa wageni," akiongeza kuwa, tangu wakati huo, maajinabi wamekuwa wakitaka kurejesha hali zilizokuwa zikiendelea.

"Taifa la Iran limesimama kidete na kwa uthabiti," Imam Khamenei amesema na kusisitiza kuwa, "Nembo ya uthabiti huu ni Bahman 22." Amesema mikusanyiko hiyo ya kila mwaka "haina kifani" duniani kote, akibainisha kuwa, hakuna mfano mwingine wa taifa linaloadhimisha uhuru wake kila mwaka kwa ushiriki mkubwa kama huo wa kitaifa.

Maandamano hayo "yatawalazimisha wale wanaoimezea mate Iran na maslahi yake kusalimu amri," Ayatullah Khamenei amesema na kueleza kuwa, "Nguvu ya kitaifa inahusiana zaidi na matakwa ya mataifa na uthabiti wao kuliko makombora na ndege,"  akiwahimiza wananchi kuendelea kuonyesha azma yao katika nyanja mbalimbali.

"Wakatisheni tamaa maadui," Kiongozi Muadhamu amesema, akisisitiza kwamba taifa hili linabaki katika hatari, madhali tu maadui wake hawatakatishwa tamaa. Imam Khamenei amesema umoja, nia thabiti, motisha, na upinzani dhidi ya vishawishi vya adui ndio nguzo za nguvu ya taifa.

Ayatullah Khamenei pia alielezea matumaini kwamba vijana wa Iran watasonga mbele katika sayansi, vitendo, uchamungu, maadili, na maendeleo ya kimwili na kiroho, na hivyo kujenga fahari kwa nchi.

Alisema Februari 11 inaonyesha sifa hizi zote, huku watu wakijitokeza mitaani kuonyesha umoja, uaminifu kwa Jamhuri ya Kiislamu, na kujitolea kwa taifa. Kiongozi Muadhamu ameonyesha matumaini kwamba mikusanyiko na matembezi ya mwaka huu yataongeza zaidi izza ya taifa la Iran, kama ilivyokuwa miaka iliyopita.