Iran yahimiza kufukuzwa Israel katika Tume ya Umoja wa Mataifa ya Wanawake
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i119544-iran_yahimiza_kufukuzwa_israel_katika_tume_ya_umoja_wa_mataifa_ya_wanawake
Katibu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Iran, ameitaka Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya Wanawake (UNCSW) kuiondoa Israel katika jumuiya hiyo ya kimataifa kutokana na vita vyake vya umwagaji damu na uhalifu wa kutisha dhidi ya wanawake na wasichana katika Ukanda wa Gaza na Lebanon.
(last modified 2024-11-30T09:44:18+00:00 )
Nov 30, 2024 09:44 UTC
  • Iran yahimiza kufukuzwa Israel katika Tume ya Umoja wa Mataifa ya Wanawake

Katibu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Iran, ameitaka Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya Wanawake (UNCSW) kuiondoa Israel katika jumuiya hiyo ya kimataifa kutokana na vita vyake vya umwagaji damu na uhalifu wa kutisha dhidi ya wanawake na wasichana katika Ukanda wa Gaza na Lebanon.

Kazem Gharibabadi, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya sheria na kimataifa, ameeleza hayo katika barua nne tofauti alizowaandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, Rais wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa, Bob Rae, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya uchumi wa wanawake, Abdulaziz M. Alwasil, na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk.

"Kuwepo utawala mtendajinai wa Kizayuni ambao taasisi za kimataifa za haki za binadamu, wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa na wanaharakati huru wa haki za binadamu, wanasema umeifanya Gaza kuwa machinjio ya raia, hususan wanawake na watoto, katika Tume ya Umoja wa Mataifa ya Hali ya Wanawake, ambayo asili yake ni kukuza haki za wanawake na wasichana na kuzuia unyanyasaji na ubaguzi dhidi yao, kunahitimisha kabisa uaminifu wa taasisi za kimataifa na matarajio ya watu kwa kazi za taasisi hizo nyakati za migogoro na vitisho dhidi ya binadamu," ameandika Gharibabadi.

Gharibabadi

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Utawala unaoua watoto wa Kizayuni unaua mtoto mmoja huko Gaza kila baada ya dakika 10. Zaidi ya watoto 17,000 wa Kipalestina wameuawa shahidi hadi sasa katika mauaji hayo ya kikatili, na zaidi ya watoto 255,000 wa Kipalestina huko Gaza wamepoteza baba au mama zao."

Gharibabadi ameashiria pia hali mbaya ya wanawake wa Lebanon hususan wajawazito kutokana na uvamizi na mashambulizi ya Israel dhidi ya majengo ya makazi ya watu na kusema kuwa, kuhama na uharibifu unaosababishwa na mashambulizi makali ya mabomu vimezidisha matukio ya kuharibika kwa mimba, kuzaa watoto kabla ya wakati na watoto wafu na kuongeza kwa kiasi kikubwa hatari ya vifo vya uzazi.

Amesisitiza kuwa: "Kwa kuzingatia jinai zake za kutisha na za kinyama, hususan dhidi ya wanawake na watoto, ni wazi kabisa kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel haupaswi kamwe kuruhusiwa kuwa na kiti au kujiunga tena na taasisi za haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Hali ya Wanawake.”