Iran: Njama za Wamarekani na Wazayuni nchini Syria zinalenga kuyumbisha Asia Magharibi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi anasema kuibuka tena ugaidi wa kitakfiri kaskazini mwa Syria ni sehemu ya mradi wa Marekani na Israel unaolenga kueneza ukosefu wa usalama katika eneo la Asia Magharibi.
Katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov siku ya Jumamosi, Araghchi alisema jamii ya kimataifa inabeba jukumu la kupambana na janga hilo baya la ugaidi.
Ameongeza kuwa Iran, Russia na nchi za kieneo, hususan nchi jirani za Syria, lazima ziendelee kuwa macho na kuboresha ushirikiano ili "kuzuia njama hii hatari na kukabiliana na hatua za magaidi nchini Syria."
Waziri wa mambo ya nje wa Russia, kwa upande wake, amemueleza mwenzake wa Iran kuhusu tathmini yake ya matukio ya hivi karibuni nchini Syria.
Lavrov ametoa wito kwa pande zote kuchukua hatua zilizoratibiwa zaidi za kukabiliana na ugaidi na akahimiza mashauriano ya karibu kati ya Tehran na Moscow.
Wanadiplomasia hao wa ngazi za juu zaidi wa Iran na Russia wamethibitisha tena uungaji mkono thabiti wa nchi zao kwa mamlaka ya kitaifa ya Syria na pia serikali na jeshi la nchi hiyo ya Kiarabu katika mapambano yao dhidi ya makundi ya kigaidi.
Kundi la kigaidi la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) na makundi washirika yake ya kigaidi yaliingia katika sehemu za mji wa pili kwa ukubwa nchini Syria wa Aleppo siku ya Ijumaa, na kuyateka maeneo kadhaa yakiwemo ya al-Hamdaniyah, al-Furqan na al-Zahraa baada ya siku mbili za mapigano makali. Vikosi vya Syria vimeanzisha haraka operesheni za kukabiliana na magaidi hao wanaopata himaya ya kigeni.