Iran: Troika ya Ulaya inapasa kukomesha mara moja vitendo vinavyokiuka JCPOA
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amemtumia barua Katibu Mkuu wa umoja huo na Baraza la Usalama akisema kuwa tuhuma zilizotolewa dhidi ya Tehran hazina msingi wowote na zina malengo ya kisiasa. Amir Saeid Iravani ameeleza haya kufuatia tuhuma zilizotolewa na wawakilishi wa Troika ya Ulaya dhidi ya Tehran.
Wawakilishi wa kudumu wa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza katika Umoja wa Mataifa wameituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa haifungamani na ahadi na ahadi zake kwa mujibu wa mapatano ya JCPOA na kwamba imekiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama.
Amir Saeid Iravani Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran UN mjini New York ametuma barua kwa Baraza la Usalama na kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na kuyataja madai ya Troika ya Ulaya kuwa hayana msingi na ni ya upotoshaji. Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechukua hatua katika fremu ya haki halali zilizoorodheshwa katika vipengee vya 26 na 36 vya mapatano ya JCPOA na katika kujibu hatua ya upande mmoja ya Marekani ya kujitoa katika mapatano hayo.
Barua ya Balozi wa Iran UN imebainisha kuwa: Troika ya Ulaya imekiuka ahadi zake katika kuondoa vikwazo na imeendeleza sera zake za uhasama kwa kuweka vikwazo vipya ikiwemo vikwazo dhidi ya njia za meli za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na sekta ya anga.
Katika barua hiyo, Iravani pia ameashiria ushirikiano wa wazi na athirifu wa Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kusisitiza kuwa miradi ya nyuklia ya Iran inasimamiwa kikamilifu kwa mujibu wa mkataba wa NPT, na kuwa silaha za nyuklia hazina nafasi yoyote katika mfumo wa ulinzi wa Iran.