Iran yasema: Marekani na Israel zinachochea ugaidi wa kitakfiri nchini Syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amezilaumu Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa ongezeko la ugaidi hivi karibuni kaskazini mwa Syria na kuitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua za haraka na madhubuti za kukabiliana na kuibuka tena magenge ya kigaidi ya ukufurishaji katika taifa hilo la Kiarabu.
Araghchi aliyasema hayo jana Jumanne katika kikao cha 28 cha Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi (ECO) katika mji wa Mashhad, kaskazini mashariki mwa Iran.
Ameongeza kuwa, Asia Magharibi na dunia nzima imekuwa ikishuhudia ukatili usio na kikomo wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao haujawahi kushuhudiwa na wa kutisha dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza kwa zaidi ya mwaka mmoja, na pia jinai dhidi ya taifa la Lebanon.
Amelaani harakati mpya za makundi ya kigaidi ya kitakfiri nchini Syria kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon na Israel, akisema magaidi hao wamejipanga upya kwa uungaji mkono unaotolewa na Marekani na utawala wa Tel Aviv.
Magaidi wanaoungwa mkono na Marekani, utawala haramu wa Israel na waitifaki wao, wakiongozwa na kundi la Takfiri la Hayat Tahrir al-Shams (HTS) walifanya shambulio la kushtukiza katika majimbo ya Aleppo na Idlib wiki iliyopita, na kuteka idadi ya vijiji na miji kabla ya kuingia Aleppo tarehe 27 Novemba.
Syria imekuwa ikikabiliana na magaidi na waasi wanaofadhiliwa na mataifa ya kigeni tangu Machi 2011. Damascus imezikosoa nchi Magharibi na washirika wao wa kieneo kwa kuyasaidia makundi ya kigaidi kuleta uharibifu katika nchi za Kiarabu.