Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran aelekea Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i119782-waziri_wa_mashauri_ya_kigeni_wa_iran_aelekea_iraq
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo ameelekea Baghdad mji mkuu wa Iraq ikiwa ni muendelezo wa safari yake ya kieneo yenye lengo la kujadili matukio ya hivi karibuni nchini Syria na eneo la Asia Magharibi kwa ujumla.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Dec 06, 2024 03:58 UTC
  • Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran aelekea Iraq

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo ameelekea Baghdad mji mkuu wa Iraq ikiwa ni muendelezo wa safari yake ya kieneo yenye lengo la kujadili matukio ya hivi karibuni nchini Syria na eneo la Asia Magharibi kwa ujumla.

Akiwa mjini Baghdad Sayyid Abbas Araghchi atashiriki katika mkutano wa pamoja na Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iraq na Syria utakaochunguza matukio ya hivi majuzi ya kisiasa na kiusalama katika eneo hili.

Kukutana na viongozi wa Iraq na kupitia upya uhusiano wa pande mbili kati ya Tehran na Baghdad ni lengo jingine la Abbas Araghchi katika safari hii ya Iraq.

Katika safari hii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Araghchi atakutana na kufanya mashauriano na mwenzake wa Iraq, Fouad Hossein, na kisha atakuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu Mohammad Shia al-Sudani na Rais wa Iraq Abdul Latif Rashid.

Kabla ya kuelekea Iraq, Abbas Araghchi alifanya safari katika mataifa ya Syria na Uturuki na kukutana na mawaziri wenzake wa mashauri ya kigeni ambapo sambamba na kujadili matukio ya hivi karibuni alibadilishana mawazo na wenyeji wake kuhusiana na matukio ya sasa ya Syria pamoja na uhusiano wa pande mbili.