Iran yakanusha uvumi wa kufunga ubalozi wake mjini Damascus Syria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i119842-iran_yakanusha_uvumi_wa_kufunga_ubalozi_wake_mjini_damascus_syria
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amepuuzilia mbali uvumi unaodai kuwa Tehran imefungwa Ubalozi wake nchini Syria kufuatia kuibuka tena makundi ya wanamgambo wenye silaha nchini humo.
(last modified 2024-12-07T08:09:29+00:00 )
Dec 07, 2024 08:09 UTC
  • Iran yakanusha uvumi wa kufunga ubalozi wake mjini Damascus Syria

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amepuuzilia mbali uvumi unaodai kuwa Tehran imefungwa Ubalozi wake nchini Syria kufuatia kuibuka tena makundi ya wanamgambo wenye silaha nchini humo.

Esmail Baghaei ametangaza habari hiyo leo Jumamosi na kusisitiza kuwa, madai ya vyombo vya habari vya Magharibi kuhusu kuondolewa wafanyakazi wa Ubalozi wa Iran katika mji mkuu wa Syria ni za uongo na kwamba ubalozi huo unaendelea na kazi zake kama kawaida.

Katika ripoti yake jana Ijumaa, gazeti la The New York Times la Marekani lilieneza uvumi kuwa Iran imeanza kuhamisha wanadiplomasia wake na familia zao mjini Damascus huku vikosi vya serikali ya Syria vikiendelea kupambana na wanamgambo wanaoipinga Damascus.

Mapema jana Ijumaa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi alisema kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel na makundi ya washirika wake wanataka kuigeuza Syria kuwa kituo cha "ugaidi na tishio" la usalama wa eneo zima la Asia Magharibi.

Araghchi, alisisitiza kwamba Iran itaendelea kuiunga mkono serikali na taifa la Syria. Amesema: "Tutaendeleza msaada wetu kwa msingi wa kutekeleza kila ambacho Damascus inataka kutoka kwetu."