Araghchi: Ilishangaza namna Jeshi la Syria lilishindwa kukabiliana na wanamgambo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i119910-araghchi_ilishangaza_namna_jeshi_la_syria_lilishindwa_kukabiliana_na_wanamgambo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema kwamba Jamhuri ya Kiislamu ilikuwa imeifahamisha serikali ya Syria kuhusu mashambulio yaliyokuwa yakipangwa na wanamgambo kabla hayajaanza.  Ameongeza kuwa imeshangaza jinsi Jeshi la Syria lilipoteza uwezo wa kukabiliana na mashambulizi hayo yaliyokuwa na kasi kubwa.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Dec 09, 2024 04:38 UTC
  • Araghchi: Ilishangaza namna Jeshi la Syria lilishindwa kukabiliana na wanamgambo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema kwamba Jamhuri ya Kiislamu ilikuwa imeifahamisha serikali ya Syria kuhusu mashambulio yaliyokuwa yakipangwa na wanamgambo kabla hayajaanza.  Ameongeza kuwa imeshangaza jinsi Jeshi la Syria lilipoteza uwezo wa kukabiliana na mashambulizi hayo yaliyokuwa na kasi kubwa.

Araghchi aliyasema hayo Jumapili katika mahojiano na televisheni ya Iran kufuatia kuanguka kwa serikali ya Syria baada ya mashambulizi ya wanamgambo waliokuwa wakiongozwa na kundi la Hay’at Tahrir al-Sham (HTS) ambao jana walichukua udhibiti wa mji mkuu Damascus.

Araghchi amedokeza kwamba katika mkutano wake wa hivi karibuni na Rais Bashar al-Assad, kiongozi huyo aliyetimuliwa, rais huyo alilalamika kuhusu hali mbaya ya jeshi lake.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kwamba wajibu mkuu wa kulinda nchi uko mikononi mwa jeshi la Syria, na Iran haikuwa na jukumu katika suala hilo.

Aragchi amesema moja ya mapendekezo ya Iran kwa serikali ya Syria daima yalikuwa kuhimiza  mazungumzo na mwingiliano na vikundi vya upinzani na kujaribu kutatua masuala kwa amani bila kuumiza watu. 

Waziri wa mambo ya nje wa Iran amesema kuwa maendeleo nchini Syria hayatakandamiza harakati ya upinzani ya Lebanon, Hizbullah. Araghchi alisema kuwa silaha, vifaa na miundombinu ya Hizbullah ya sasa yanatosha kwa mapambano yake katika mwaka moja au miwili ijayo.