Iran itajibu hatua za uhasama katika sekta ya nyuklia
Iran imesisitiza kuwa haitasita kujibu hatua za uhasama zinazolenga mpango wake wa nishati ya nyuklia, lakini bado iko tayari kuendelea na ushirikiano na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).
Hayo yamedokezwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi siku ya Jumatatu wakati wa mazungumzo ya simu na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) Rafael Grossi.
Katika mazungumzo hayo, Aragchi aliwakosoa vikali baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Magavana wa IAEA kwa kuchukua hatua zisizo sahihi ambazo zilizuia ziara ya mwezi Novemba ya Grossi nchini Iran na hivyo kuvuruga jitihada za pande hizo mbili za kutatua masuala ambayo bado hayajakamilika kuhusu masuala ya usalama wa nyuklia.
Marekani na washirika wake wa Ulaya wanadai kuwa eti Iran haitoi ushirikiano wa kutosha kwa IAEA, ingawa ushirikiano wa Tehran na chombo hicho umeimarika na kuboreka katika miaka ya hivi karibuni.
Mnamo tarehe 21 Novemba, Bodi ya Magavana ya IAEA ilipitisha azimio, llilopendekezwa na Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani, ambalo lilirudia madai yasiyo na msingi kuhusu shughuli za nyuklia za Iran zenye malengo ya amani. Katika kujibu madai hayo Iran imeanza kuingiza gesi ya urani kwenye mashinepewa au sentrifuji za kisasa kama jibu kwa azimio la hivi karibuni la Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA).
Juzi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alieleza kuwa, mpango wa amani wa nyuklia wa Iran unatekelezwa katika fremu ya Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Nyuklia na chini ya usimamizi wa Wakala wa IAEA.