Ushauri muhimu wa Araghchi kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amesisitiza katika ushauri wake kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusu matukio ya Syria kuwa: ili kuondokana na kipindi hiki hahtari sana katika eneo hili, nchi zote zinapaswa kutumia busara, ushirikiano, kushirikishwa makundi yote, kuepuka migawanyiko na kutojali maslahi binafsi.
Katika kujibu taarifa ya hivi karibuni ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusu Syria na madai ya kuhusika Iran katika matukio ya hivi karibuni nchini humo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Kama mlivyo nyinyi, sisi pia tunataka utulivu, amani na kuzuia kuzuka vurugu na machafuko nchini Syria."
Araghchi ameongeza kuwa, tuna sababu za wazi kabisa, zinazotufanya tulinde umoja wa ardhi ya Syria, kulinda usalama wa makabila, wa madhehebu na dini zote, wawe Masuni, Mashia, Maalawi, Wakurdi, Waarabu pamoja na kuhifadhiwa usalama na kuheshimu utakatifu wa maeneo matakatifu. Aidha tunapigania kupunguzwa silaha haramu, tunapinga uingiliaji wowote wa kigeni kwa kisingizio chochote kile, kuzuia Syria kuwa kimbilio na maficho ya vitendo vya kigaidi, itikadi kali na vurugu. Tunataka ili Syria isiwe tishio kwa majirani zake na eneo hili lote. Tunapigania kuzuia matukio zaidi na kijinai ya Israel na tunataka pia kuundwe serikali na utawala jumuishi nchini Syria.
Kwa upande wake, Esmail Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amekumbusha misimamo imara na ya muda wote ya Iran katika kuunga mkono uadilifu wa ardhi na umoja wa kitaifa wa Syria na kuundwa utawala jumuishi wa kisiasa kupitia kushirikishwa mirengo yote ya kisiasa na kikabila na watu wa dini zote sambamba na kulindwa haki za walio wachache na kuheshimiwa maeneo matakatifu.
Mfumo wa kisiasa wa Syria uliokuwa unaongozwa na Rais Bashar al-Assad ulianguka tarehe 8 Disemba, 2024. Makundi ya upinzani na magenge ya kigaidi yaliyoungwa mkono na Marekani na utawala wa Kizayuni na Uturuki yalifanikiwa kuiangusha serikali ya Bashar al-Assad. Hivi sasa, vyombo vya habari vinavyoupinga utawala wa zamani wa Syria vinajaribu kuchora na kuakisi sura mbaya ya utawala wa Bashar al Assad na kuupamba kisasa utawala wa hivi sasa wa nchi hii kwa kutumia propaganda nzito. Vyombo hivyo vinajaribu kuonesha utawala mpya ni wa watu wanaoheshimu imani za walio wachache, wanaopinga ghasia na wanaojali maendeleo na ustawi wa watu. Hata hivyo, tangu siku za kwanza kabisa, ilikuwa wazi kwamba propaganda hizo zinapingana na ukweli halisi kuhusu uhalisia wa magenge hayo ya kigaidi.
Kwa kuzingatia matukio ya eneo hili na hali mpya iliyojitokeza nchini Syria, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nayo inaendelea kutilia mkazo mikakati yake ya kuanzishwa mazungumzo ya kitaifa kati ya wananchi wenyewe wa Syria ili pande zote zishirikishwe katika utawala na kulindwa haki zake. Iran imependekeza kufanyike mkutano katika ngazi ya kimataifa; kwa kushirikishwa nchi zote za wafadhili kwa ajili ya ujenzi mpya wa Syria.
Wakati huo huo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa, kama ilivyo kwa fitna na migogoro mingine yote ya eneo hili, hivi sasa pia Marekani na utawala wa Kizayuni ndio chanzo kikuu cha matatizo ya hivi sasa nchini Syria hasa kwa kuzingatia kuwa, matatizo ya leo ya Syria ni moja ya malengo makuu ya utawala wa Kizayuni wa Israel, ambayo ni kujitanua na kupora ardhi za mataifa mengine.
Kwa kuzingatia yote hayo ni lazima nchi jirani, hususan nchi za Kiislamu na pia taasisi za kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama, kulinda haki ya kujitawala taifa la Syria, kurejesha amani na utulivu na pia kukomboa ardhi zote za Syria na kuzirudisha kwa wananchi wenyewe wa nchi hiyo ya Kiarabu na Kiislamu.