Kiongozi Muadhamu: Lazima tuwe wabunifu katika upashaji wetu wa habari
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametoa ujumbe muhimu kuhusu udharura wa kuvitumia vizuri vyombo vya habari na vya mawasiliano ya umma hasa wakati huu wa vita vya kila upande baina ya haki na batili.
Katika ujumbe wake huo kwa kwa Kikao cha Upeo wa Mabadiliko ya Chombo cha Habari cha Taifa (IRIB), Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia nafasi isiyo na mbadala ya vyombo vya habari katika mapambano ya hivi sasa ya haki na batili duniani na kusema: Ni lazima tufanye jitihada maradufu katika tasnia ya vyombo vya habari ili tuweze kuzalisha habari kwa usahihi mkubwa zaidi.
Ujumbe huo wa Kiongozi Muadhamu umesomwa mbele ya mkuu wa maafisa wengine wa ngazi za juu wa Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB na kusisitiza kuwa, shirika la IRIB lina uwezo mkubwa wa kufikisha ujumbe na taarifa za kweli kwa walimwengu na hiyo ni silaha muhimu zaidi kabla ya silaha za kijeshi katika kuainisha mshindi kwenye medani ya mapambano. Hivyo ametaka kuweko umakini zaidi, jitihada kubwa zaidi na ubunifu zaidi kwenye chombo hicho muhimu mno cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Matini ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Allah Mtukufu
Mheshimiwa mpendwa Jebeli (Mkuu wa shirika la IRIB)
Wewe pamoja na waungwana hawa wengine wote mnalijua jukumu lisilo na mbadala la vyombo vya habari na tablighi katika mapambano ya hivi sasa ya ulimwengu. Umuhimu huo ni mkubwa zaidi hivi sasa kuliko huko nyuma. Leo hii ushindi ni wa upande ambao una nguvu za kuchukua na kufikisha ujumbe na taarifa kuhusu uhalisia wa kitu fulani; na athari ya jambo hilo ni muhimu na kubwa zaidi kabla ya kuingizwa zana za kijeshi katika medani ya vita. Sisi katika uwanja huu muhimu lazima tuwe makini, tufanye jitihada kubwa na tuwe wabunifu zaidi. Huu ndio ujumbe wangu kwa kongamano hilo,
Sayyid Ali Khamenei.