Iran yajikarabatia kikamilifu ndege ya Airbus licha ya vikwazo vya Magharibi
Iran imesema moja ya ndege zake za Airbus ambazo zimesimamishwa kutokana na vikwazo vya Marekani imeanza tena kuruka angani kutokana na juhudi za wahandisi wa ndani za kutengeneza au kukarabati vipuri vinavyohitajika.
Kwa mujibu wa Shirika la habari la ILNA, Shrika la Ndege la Qeshm Air la Iran limetangaza kuwa limeweza kukidhi vigezo vyote vya kiufundi vya Shirika la Airbus kwa ajili ya mfumo wa kutua wa moja ya ndege zake za Airbus 300-600.
Mafanikio hayo yalitokana na mradi wa pamoja wa timu ya wataalamu wa kiufundi na uhandisi wa Qeshm Air na idara ya kiufundi na uhandisi ya Shirika la Kitaifa la Ndege la Iran, maarufu kama Iran Air.
Tamko hilo limeyataja mafanikio hayo kuwa ni "hatua inayong'ara kwenye njia ya kujitosheleza katika sekta ya anga ya Iran." Ndege hiyo ya Airbus sasa iko tayari kufanya safari za kimataifa kutoka uwanja wa ndege wa Imam Khomeini mjini Tehran.

Iran iliwekewa vikwazo vipya vya Marekani mnamo mwaka 2018 baada ya Washington kujiondoa peke yake kwenye makubaliano ya kimataifa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yanayojulikana kama JCPOA.
Hata hivyo, Iran imeweza kujikarabatia ndege zake licha ya vikwazo vinavyoizuia kupata teknolojia ya kigeni na vipuri vya ndege.
Iran imepiga hatua katika uwanja huo kiasi kwamba sasa inatoa huduma za matengenezo ya ndege kwa mashirika ya ndege ya kigeni.
Shirika la habari la Reuters liliripoti mwezi Aprili mwaka jana kwamba shirika kubwa zaidi la ndege la Russia, Aeroflot, lilituma moja ya ndege zake zilizoundwa Magharibi kufanyiwa matengenezo nchini Iran.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Iran ilisema mwezi uliopita kwamba Iran imeweza kumiliki teknolojia inayohitajika kutengeneza vipuri vya injini za ndege za Boeing na Airbus.