Wairani wanadhimisha kumbukumbu ya miaka 5 ya kuuawa shahidi Jenerali Soleimani
Makumi ya maelfu ya wananchi wa Iran wamemiminika katika mkoa wa kusini mashariki wa Kerman kutoa heshima kwa kamanda mkuu wa kupambana na ugaidi, Jenerali Qassem Soleimani.
Leo Alhamisi, katika mji aliozaliwa na eneo la kaburi la Jenerali Soleimani, kumeshuhudiwa mafuriko ya maashiqi na wapenzi wa kamanda huyo mashuhuri huku kukiwa na baridi kali na theluji wakati huu wa kumbukumbu ya miaka mitano ya kuuawa kwake shahidi.
Katika miji mingine ya Iran, ukiwemo mji mkuu, Tehran, kulikuwa na mijumuiko mbalimbali ya kumkumbuka Jenerali Soleimani.
Jenerali Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) na Abu Mahdi al-Muhandis, mkuu wa Kitengo cha Uhamasishaji cha Iraq (PMU) na wanamapambano wenzao waliuawa shahidi katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani Januari 3, 2020 karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad. Shambulizi hilo la kigaidi liliidhinishwa na Rais wa wakati huo wa Marekani, Donald Trump.
Makamanda hao wawili walikuwa wakiheshimika sana katika eneo la Asia Magharibi na duniani kote kwa sababu ya jukumu lao muhimu katika kupambana na kundi la kigaidi la Daesh katika eneo hilo hususan Iraq na Syria.
Katika muda wa chini ya wiki moja baada ya shambulio hilo, wabunge wa Iraq waliidhinisha muswada ulioitaka serikali kuwafukuza wanajeshi wote wa kigeni wanaoongozwa na Marekani nchini humo.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran pia lilitwanga kambi ya Marekani ya Ain al-Asad katika mkoa wa magharibi wa Anbar nchini Iraq kulipiza kisasi mauaji ya Jenerali Soleimani.