Kamanda: Majeshi ya Iran yako tayari kukabiliana na hujuma yoyote
-
Brigedia Jenerali Kioumars Heydari
Kamanda wa Vikosi vya Nchi Kavu vya Jeshi la Iran amesisitiza kuwa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu litakabiliana na hujuma yoyote dhidi ya ardhi ya nchi.
Brigedia Jenerali Kioumars Heydari aliyasema hayo Jumamosi alipokuwa akitembelea maeneo ya mpaka wa Magharibi mwa nchi, ambapo amefanya ziara ya kutembelea Kikosi cha 41 cha Kikosi cha Mashambulizi kikiwemo Kitengo Maalum cha 35 cha kikosi hicho. Akiwa hapo amekagua uwezo na utayari wa mapambano wa wanajeshi walio katika eneo hilo.
"Vikosi vya Jeshi la nchi yetu, hasa Vikosi vya Nchi Kavu , vinazuia aina yoyote ya uvamizi dhidi ya ardhi ya taifa letu la Kiislamu kwa kutegemea azma ya kitaifa," alisema.
Brigedia Jenerali Heydari amesisitiza umuhimu mkubwa wa vikosi vya kijeshi kutii uongozi wa kidini, akielezea uaminifu kwa uongozi kama sababu "inayoongoza katika kumpkonya adui silaha na ni ngao yenye nguvu zaidi dhidi yao."
Pia alisisitiza juu ya asili ya lazima ya kuzingatia haki na ustahiki katika vikosi vyote.
Matamshi hayo yametolewa wakati kukiwa na maneva ya kijeshi yanayoendelea katika maeneo ya Magharibi mwa Iran yanayotekelezwa na Kikosi cha Nchi Kavu vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchi hiyo (IRGC).
Vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu vimekuwa vikiendelea kuimarisha vifaa vyao vya kijeshi na utayari wa mapambano kwa mujibu wa maagizo ambayo yametolewa na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei.
Vikosi vya kijeshi vya Iran hufanya mazoezi ya mara kwa mara kulingana na ratiba ya kina katika sehemu mbalimbali za nchi ili kujaribu silaha zao na vifaa na kutathmini utayari wao wa kivita.
Maafisa wa nchi Iran wamesisitiza mara kwa mara kwamba nchi haitasita kuimarisha uwezo wake wa kijeshi, ikiwa ni pamoja na nguvu zake za makombora, ambazo zinalenga kabisa kujihami, na kwamba uwezo wa ulinzi wa Iran hautawahi kuwa sehemu ya mazungumzo.