Iran yalaani mripuko mbaya wa bomu uliotokea Baluchistan Pakistan
Iran imelaani vikali shambulio baya lililolenga msafara wa magari yaliyokuwa yamebeba wanajeshi na wafanyakazi katika jimbo la Baluchistan la kusini magharibi mwa Pakistan.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei ametoa mkono huo wa pole leo Jumapili kwa familia zilizopoteza wapendwa wao pamoja na kwa serikali ya Pakistan na kwa wananchi wote wa nchi hiyo kufuatia kutokea shambulio hilo la kigaidi akisisitizia haja ya kuimarishwa juhudi za kuzuia mashambulizi hayo na kupambana na ugaidi kwa ari na nguvu kubwa zaidi.
Ripoti zinasema kuwa mripuko huo ulitokea Jumamosi katika mji wa Turbat, wakati msafara wa wanajeshi wa Pakistan ulipokuwa unasindikiza magari ya Kikosi cha Mipaka (FC). Basi lililokuwa limebeba wafanyikazi wa FC lilishika moto baada ya shambulio hilo ambalo pia limeharibu magari mawili ya kiraia na pikipiki mbili.
Afisa mkuu wa utawala wa mkoa huo ambaye hakutaka kutajwa jina kwa sababu si msemaji rasmi amesema kuwa, wanajeshi watano wameuawa katika shambulio hilo, ambalo pia lilijeruhi karibu watu wengine 40 wakiwemo raia. Kundi la wanamgambo wa Baloch Liberation Army (BLA) limedai kuhusika na mripuko huo wa bomu.
Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif amelaani vikali shambulizi hilo na kuwaombea dua za kheri, marehemu na majeruhi.
Katika taarifa yake kwa taifa, Shehbaz Sharif amesema: "Magaidi hawatofanikiwa kufikia malengo yao machafu. Serikali na vikosi vya usalama (vya Pakistan) vinafanya kazi kwa bidii kubwa kupambana na magaidi hao. Kuna azma thabiti ya kumaliza kabisa vitendo vya kigaidi nchini Pakistan.”