Iran: Tuna silaha ambazo adui kamwe hawezi kuzitasawari
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i121374-iran_tuna_silaha_ambazo_adui_kamwe_hawezi_kuzitasawari
Kamanda mmoja wa ngazi za juu wa Jeshi la Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ina silaha ambazo hazijafichuliwa hadi sasa na wala adui hana taarifa zozote kuhusu silaha hizo.
(last modified 2025-01-13T03:13:25+00:00 )
Jan 13, 2025 03:13 UTC
  • Iran: Tuna silaha ambazo adui kamwe hawezi kuzitasawari

Kamanda mmoja wa ngazi za juu wa Jeshi la Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ina silaha ambazo hazijafichuliwa hadi sasa na wala adui hana taarifa zozote kuhusu silaha hizo.

Naibu Mkuu wa Majeshi ya Iran, Brigedia Jenerali Mohammad Reza Ashtiani aliyasema hayo jana Jumapili alipokuwa akizungumzia mazoezi ya kijeshi ya  Jeshi la Iran kwa ajili ya kuonesha ustadi na utayari wake wa kukabiliana na vitisho vya adui. 

Jenerali Ashtiani ametamka hayo mbele ya waandishi wa habari na kusisitiza kwa kusema: “Tuna silaha ambazo hatujawahi kuzizungumzia hadi sasa na adui hana taarifa zozote kuhusu silaha hizo. Baadhi ya silaha hizo zinaweza kujaribiwa wakati wa mazoezi  ya kijeshi.”

Ameongeza kuwa, Jeshi la Iran limekuwa likifanya mazoezi mara kwa mara ili kuboresha uwezo wake wa kivita katika nyuga mbalimbali na kuhakikisha kuwa usalama wa taifa hili unalindwa kikamilifu.

Amesema: Kama ambavyo Iran inafuatilia kwa karibuni sana mienendo ya maadui, ni hivyo hivyo inafuatilia kwa nguvu utayari na umahiri wake wa kukabiliana na vitisho. 

Amesisitiza kuwa matukio yote ya eneo hili yanafuatiliwa kwa karibu mno na vikosi vya ulinzi vya Iran na kwamba Jamhuri ya Kiislamu huwa inatoa majibu makali kwa misimamo ya kuchupa mipaka, mihemko na dhana potofu ambazo adui wa taifa la Iran anaweza kuwa nazo.

Matamshi ya Ashtiani ameyatoa kwa mnasaba wa kuanza mazoezi ya kijeshi ya Egtedar 1403 ya jeshi la Iran kwa ajili ya ulinzi wa anga wa maeneo ya magharibi na kaskazini mwa Iran ikiwa ni pamoja na Fordow na Khondab ambayo yana vinu vya nyuklia vya kurutubisha madini ya urani na maji mazito.