Baqaei: Utawala wa Kizayuni hauna mipaka katika tamaa zake
-
Ismail Baqaei
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa, utawala haramu wa Israel unaotenda jinai za kutisha huko Gaza hauna mpaka wala mwisho katika taamaa zake za kujitanua.
Ismail Baqaei amesema hayo katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari na kueleza kwamba, mtazamo unaofuatwa na utawala wa Kizayuni unaeleza matamanio yake kuhusu eneo hili na uanzishaji wake wa mipango inayojumuisha maeneo mengine ya eneo hili, kama vile Syria, Jordan, Lebanon, na takriban Palestina yote inayokaliwa kwa mabavu.
Amesisitiza kuwa, hatua hizi ni ishara ya wazi kabisa kwamba, utawala wa Kizayuni hauna wala haufahamu kikomo katika siasa zake za kujitanua.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameongeza kuwa, Israel imekiuka mara mia makubaliano ya kusitisha vita huko Lebanon na kupuuza kikamilifu majukumu yake.
Kadhalika Baqaei amesema, utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya mauaji ya halaiki huko Gaza ndani ya miezi kumi na sita, na kueleza kuwa hii ni fedheha kwa ulimwengu na mashirika ya kimataifa.
Akitoa tathmini yake kuhusu matukio ya Syria, Ismail Baqaei amesema: Mustakabali wa uhusiano wa Iran na Syria unategemea utendaji wa upande wa pili.