Iran leo inaadhimisha kuzaliwa Imam Ali (as) na Siku ya Baba
Iran, leo tarehe 13 mwezi Rajab, inaadhimisha Siku ya Baba katika sherehe zinazofungamanishwa na kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa Amirul Muuminina, Imam Ali bin Abi Twalib (as).
Siku ya kuzaliwa Imam Ali (as) imepewa jina la Siku ya Baba, ili kutambua mchango wa baba katika familia na jamii, kujitolea kwa akina baba na majukumu yao kama nguzo za maisha ya familia, suala ambalo lina mizizi katika mafundisho ya Kiislamu na utamaduni wa Iran.
Katika utamaduni wa Kiislamu, jukumu la baba linatambuliwa kuwa msingi wa utulivu wa familia na jamii.
Katika mila na utamaduni wa Iran pia, akina baba wanaheshimiwa kama nembo ya hekima, mamlaka na kujisabilia.
Siku ya Baba inasadifiana na kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Ali (as), kielelezo cha kudumu cha uadilifu, upendo, na ubaba usio na kifani katika historia ya Kiislamu. Akijulikana kwa ushujaa na hekima yake, Imam Ali (as) pia anaadhimishwa kwa nafasi yake kuu katika kutoa malezi kama baba. Historia inasimulia maingiliano yake ya upendo na watoto wake, ikimdhihirisha kama mfano wa ubaba wenye upendo na huruma.
Chaguo la kuoanisha Siku ya Taifa ya Baba na kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Ali bin Abi Twalib (as) linaonyesha muungano mkubwa wa maadili ya kidini na kitamaduni katika jamii ya Iran.
Nchini Iran, familia zinaadhimisha siku hii kwa watoto na akina mama kuwapa baba zao zawadi za aina mbalimbali zikiwemo kazi za kutengeneza kwa mikono, vitabu au mashada ya maua, na mara nyingi familia hukutana nyumbani kwa baba na kupata chakula kwa pamoja.

Imam Ali bin Abi Twalib, Swahaba wa karibu zaidi kwa Mtume Muhammad (saw) na Imam wa kwanza wa Waislamu katika kizazi chake, alizaliwa tarehe 13 Rajab katika Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba. Mama wa mtukufu huyo ni Bibi Fatima bint Assad na baba yake ni Abu Talib.
Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji asiye na mithili, lakini Imam Ali bin Abi Talib alikuwa mpole, mwingi wa huruma na mtetezi wa wanyonge.