Iran na nchi tatu za Ulaya zakubaliana kuanzisha mazungumzo ya kuondoa vikwazo
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusiaka na Masuala ya Kisheria ametangaza habari ya kufikiwa makubaliano bainaya Iran na nchi tatu za Ulaya kwa ajili ya kuanzisha mazungumzo ya kuondoa vikwazo.
Gharibabadi, ameandika kwenye Mtandao wa X kwamba: Duru ya tatu ya mazungumzo kati ya Iran na nchi tatu za Ulaya (Uingereza, Ufaransa, Ujerumani) imefanyika mjini Geneva Uswisi.
Amesema: "Mazungumzo hayo yalikuwa mazito, ya wazi na ya maana. Mambo mbalimbali yamejadiliwa na kupitiwa upya katika maeneo mawili ya kuondoa vikwazo na masuala ya nyuklia ambayo ni muhimu kwa ajili ya kufikiwa mapatano baina ya pande mbili."
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala Sheria na ya Kimataifa pia ameandika: "Kumefikiwa maafikiano kwamba mazungumzo yaanzishwe tena na ili kufikia makubaliano na inabidi kuandaliwe mazingira yanayofaa na pande zote ili kuweza kuanzisha mazungumzo hayo."
Kabla ya hapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alikuwa amesema kwamba, Tehran iko tayari kufanya mazungumzo ya maana na ya haraka kuhusu mpango wake wa nyuklia.
Akizungumzia historia ya mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi alisema: "Tulifanya mazungumzo na nchi za P5+1 kwa nia njema kwa zaidi ya miaka miwili na hatimaye kufanikiwa kufikia makubaliano ambayo dunia nzima iliyakubali na kuyasifu kuwa ni mafanikio ya kidiplomasia, lakini... Marekani iliamua kujitoa bila ya sababu yoyote na kukwamisha kila kitu."