Rais Pezeshkian: Iran iko tayari kwa mazungumzo lakini itampondaponda adui iwapo itashambuliwa
Matamshi ya Rais Masoud Pezeshkian katika mahojiano yake na televisheni ya NBC News ya Marekani yameendelea kuakisiwa katika vyombo vya habari vya ndani, kikanda na kimataifa.
Katika sehemu moja ya mahojiano hayo, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian anasema Iran iko tayari kikamilifu kutoa "jibu la kuvunja meno" kwa uchokozi wowote wa adui lakini bado iko wazi kwa mazungumzo kama njia nzuri ya kusuluhisha tofauti zilizopo.
Akizungumza katika mahojiano na Lester Holt wa NBC News mjini Tehran, Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa, Iran haiogopi lakini pia haitaki vita. Amesema hayo alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kutokea mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
"Mashambulizi kama haya ya kijeshi bila shaka yatakuwa na madhara kwa kanda na ulimwengu mzima. Iran sio Gaza wala Syria. Iran ina uwezo wa kutoa jibu la kuvunja meno kwa mashambulizi kama hayo, lakini hatujawahi kuzusha mzozo katika eneo hili,” amesisitiza Rais wa Iran.
Alipoulizwa jinsi Iran itajibu iwapo Marekani na Israel zitaishambulia ili kusitisha mpango wake wa kuzalisha nishati ya nyuklia, Pezeshkian amesema, "Tutatoa majibu mwafaka kwa hatua zozote zitakazochukuliwa dhidi yetu."
"Hatuogopi vita, lakini pia hatutaki vita. Wanachozungumza ni kushambulia ardhi na vifaa, lakini tulichopata ni fikra, ujuzi na uwezo wetu ambao hauwezi kuharibiwa,” amesisitiza Rais wa Jamhuri ya Kiislamu.
Rais Pezeshkian amesema Iran iko tayari kwa mazungumzo na Marekani na Ulaya kwa kuzingatia utu, hekima na masharti sawa.