Rais Pezeshkian: Iran, Russia ziko imara katika uhusiano ‘nyeti wa kimkakati’
-
Marais Pezeshkian na Putin
Rais Masoud Pezeshkian anasema Iran na Russia zimesimama kidete katika uhusiano "nyeti, muhimu na wa kimkakati" wa pande zote.
Rais Pezeshkian ameyasema hayo katika mkutano wake na mwenzake wa Russia, Vladimir Putin mjini Moscow mapema leo Ijumaa kabla ya sherehe za kutia saini mkataba wa ushirikiano wa kimkakati unaosubiriwa kwa muda mrefu.
"Iran na Russia zinaimarisha uhusiano kila siku katika nyanja za pande mbili, kikanda na kimataifa na pia katika sekta ya uchumi na biashara," amesema Rais Pezeshkian.
Rais ameongeza kuwa makubaliano hayo ya kina yanaweza kusaidia nchi hizo mbili kuboresha uhusiano katika nyanja zote za kiuchumi, kitamaduni, kibiashara, kiusalama na mawasiliano.
Akizungumzia masuala ya kikanda, Rais Pezeshkian amesema Iran inaamini kuwa masuala ya kieneo yanapaswa kutatuliwa na nchi za eneo hili.
"Hakuna haja ya wengine kutoka upande wa pili wa dunia kuja hapa na kuvuruga eneo letu na kutekeleza sera zao," amesisitiza Rais wa Jamhuri ya Kiislamu.
Kwa upande wake, Rais Vladimir Putin amesema ziara ya hivi sasa ya Rais wa Iran na ujumbe anaofuatana nao huko Moscow ina umuhimu wa pekee kwani pande hizo mbili zimeazimia kujadili ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali na kutia saini makubaliano ya kimkakati ya ushirikiano.
Katika ziara yake mjini Moscow, Rais wa Iran anajadiliana na mwenzake wa Russia, Vladimir Putin, kuhusu suala la kupanua zaidi ushirikiano wa pande mbili, ikiwa ni pamoja na biashara, uwekezaji, usafirishaji na utamaduni, pamoja na hali ya sasa ya kikanda na masuala ya kimataifa.
Baada ya mazungumzo hayo, pande hizo mbili zitatia saini makubaliano ya ushirikiano wa kina wa kimkakati kati ya Iran na Russia.
Mkataba huo mpya wa miaka 20 unahusu maeneo ya uchumi, uchukuzi, nishati, afya na kilimo, pamoja na ushirikiano wa Tehran na Moscow katika kukabiliana na changamoto za pamoja, kupunguza athari za majanga ya kimaumbile, kupambana na uhalifu wa kupangwa, kupambana na ugaidi, na uwekezaji wa pamoja.
Iran na Russia, zinazokabiliwa na vikwazo haramu vya Magharibi, zimeimarisha ushirikiano wao katika sekta mbalimbali katika miaka ya karibuni.
Kabla ya kuelekea Russia, Rais Masoud Pezeshkian alikuwa Dushanbe huko Tajikistan ambako alifanya mazungumzo na mwenyeji wake, Emomali Rahmon, juu ya masuala yanayozihusu nchi mbili, ya kikanda na kimataifa na kusimamia hafla ya kutiwa saini hati 23 za ushirikiano katika nyanja tofauti.