Ahmad Nouruzi aipongeza taasisi ya HRF kwa kuwaandama kisheria viongozi wa Israel
Mkuu wa Kitengo cha Matangazo ya Ng'ambo cha Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) amepongeza juhudi za Taasisi ya Hind Rajab (HRF) kwa kuendesha juhudi za kimataifa za kuwafungulia mashtaka na kuwaandamana kisheria viongozi wahalifu wa Israel kwa jinai zao huko Ghaza.
Ahmad Nouruzi, ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Siku ngumu zinawangojea Wazayuni."
Kwa mujibu wa Mtandao wa Sahab, Nouruzi amefafanua zaidi kwa kuandika: "Siku ngumu zinawangojea Wazayuni. Huwezi kufanya mauaji ya kimbari huko Ghaza na kufikiri kwamba watu wenye mwamko ulimwenguni watafurahi na watakuacha ubakie salama bila ya kuandamwa."
Mwishoni mwa tweet yake hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Matangazo ya Ng'ambo cha Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) ameongeza kuwa, inabidi "tuivulie kofia" ya heshima taasisi ya HRF kwa hatua yake hiyo ya wafanya jitihada za kimataifa za kuwaburuza kizimbani viongozi watenda jinai wa Israel.
Taasisi ya Hind Rajab Foundation (HRF) ni taasisi yenye makao yake mjini Brussels Ubelgiji. Ni taasisi ya wanasheria wa haki za binadamu ambayo inapigania haki na kuwaandamana wahusika wa mauaji ya kimbari ya Ukanda wa Ghaza.
Taasisi hiyo ilianzishwa kwa heshima ya Hind Rajab, binti Kipalestina mwenye umri wa miaka sita ambaye alipigwa risasi 335 na vifaru vya Israel huko Ghaza na kuuliwa shahidi kinyama mno na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni. Hadi hivi sasa taasisi ya HRF imeshawasilisha zaidi ya mashitaka 1,100 dhidi ya wanajeshi wa Israel waliohusika katika mauaji ya umati.