Iran inapaswa kuhesabiwa kuwa mfano wa kuigwa katika kuhifadhi wakimbizi
Iran inapaswa kutambulishwa kama mfano wa kuigwa duniani katika kuhifadhi wakimbizi. Hayoi yamesema na afisa mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi nchini Iran UNHCR.
Kamishna Mkuu Msaidizi wa Operesheni wa UNHCR, Raouf Mazou aliyasema hayo katika mazungumzo yake na Mkuu wa Mkoa wa Khorasan Razavi, Gholam Hossein Mozaffari katika mji mtakatifu wa Mashhad jana Jumatano.
Ameongeza kuwa, katika nchi nyingi wakimbizi wanaishi makambini, lakini kwa hapa Iran wakimbizi wanaishi maisha ya kawaida kama raia wengine.
Amekosoa jinsi vyombo vya habari vinavyoakisi kwa udhaifu mkubwa huduma zinazotolewa na Iran kwa wakimbizi hao na kusisitiza kwamba UNHCR inapaswa kueleza hatua za Iran kwa wengine ili nchi zote duniani zichukue hatua zinazofanana.
Kwa upande wake, Mozaffari alisisitiza tena sera ya kibinadamu ya Iran kwa wakimbizi lakini akasisitiza kuwa Iran inatarajia kuungwa mkono zaidi kimataifa katika suala hili.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu, idadi kubwa ya wakimbizi wanaishi katika mazingira karibu sawa na ya raia wa Iran humu nchini.
Kwa mujibu wa ripoti ya UNHCR ya Iran ya kuanzia mwezi Aprili hadi Juni 2024, Iran ni mwenyeji wa idadi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani. Imepokea wakimbizi milioni 3.8 na watu walio na hali kama za wakimbizi na kuwahifadhi kwa ukarimu wa Iran kwa wakimbizi kwa zaidi ya miongo minne.
Ripoti ya UNHHCR ilibainisha kuwa asilimia 99 ya wakimbizi waliosajiliwa, wanaishi katika maeneo ya mijini bega kwa bega na wenyeji.