Rais wa Iran asisitiza umoja kati ya nchi za Kiislamu
Rais wa Iran amesema kuwa nchi za Kiislamu zinapasa kujiepusha na masuala yanayozusha hitilafuna badala yake zinapasa kushikama na kuwa kitu kimoja; na kwa njia hiyo ni wazi kuwa njama za maadui na wale wanaozitakia mabaya wenzao hazitafanikiwa.
Rais Masoud Pezeshkian amesema kushirikiana, maelewano na kuimarisha umoja miongoni mwa nchi za Kiislamu ni miongoni mwa mahitaji muhimu ya hali ya sasa ya dunia. Rais wa Iran amebainisha haya hapa Tehran katika mazungumzo na Mahmoud al Mashhadani Spika wa Bunge la Iraq na ujumbe anaoongozana nao ziarani hapa nchini.
Rais Pezeshkian ameashiria matukio ya karibuni katika eneo hasa huko Syria na kusema: 'Msimamo wa Iran ni kuona Syria inaunda serikali jumuishi kwa kuyashirikisha makundi yote ya wananchi, inalinda umoja wa ardhi ya nchi hiyo na inauzia kugawanywa vipande nchi hiyo.'
Rais wa Iran pia amepongeza msimamo madhubuti na wa wazi wa Iraq katika kuwahami wananchi madhulumu wa Palestina na kusema, katika uga wa kuisaidia Gaza na Lebanon tunapendekeza kuwa nchi zote za Kiislamu kwa kadiri ya uwezo wao ziwasaidie watu wa maeneo hayo katika ujenzi mpya na kurejea katika makazi yao.
Katika mazungumzo hayo, Spika wa Bunge la Iraq pia ameeleza kufurahishwa na ziara yake nchini Iran na mazungumzo aliyofanya na viongozi wa ngazi ya juu wa nchi na kusisitiza jitihada za Bunge la Iraq za kuiunga mkono serikali ya nchi hiyo katika kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi mbili.
Mahmoud al Mashhadani amesema Iraq inasisitiza kuimarisha ushirikiano wa pande mbili, wa kikanda na kimataifa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.