Iran yalaani mpango wa Marekani wa kunyakua na kuitwaa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i122390-iran_yalaani_mpango_wa_marekani_wa_kunyakua_na_kuitwaa_gaza
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amepinga vikali mpango wa Marekani wa kutaka kuinyakua na kuitwaa Gaza, na kusema kutolewa fikra kama hiyo ni jambo la kushangaza linalokwenda sambamba na mpango wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuiangamiza kabisa Palestina.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Feb 06, 2025 07:48 UTC
  • Ismail Baqaei
    Ismail Baqaei

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amepinga vikali mpango wa Marekani wa kutaka kuinyakua na kuitwaa Gaza, na kusema kutolewa fikra kama hiyo ni jambo la kushangaza linalokwenda sambamba na mpango wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuiangamiza kabisa Palestina.

Ni baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutangaza hadharani kwamba Marekani itatwaa na kuchukua udhibiti wa Ukanda wa Gaza katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, mjini Washington.

Akijibu misimamo ya hivi karibuni ya maafisa wa Marekani kuhusiana na kunyakuliwa Gaza kufuatia pendekezo la Donald Trump la kuhamishwa kwa nguvu watu wa Gaza na kupelekwa Misri na Jordan, Ismail Baqaei, amesema kuwa kutolewa fikra kama hiyo ni jambo la kushangaza na linaloendana na mpango wa utawala wa Kizayuni wa kuiangamiza kabisa Palestina. Baqaei pia  ameitaka jamii ya kimataifa kulaani mpango huo. .

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa: "Bila shaka, watu ambao wamepamba na jinai na hujuma kali zaidi za utawala ghasibu kwa muda wa miaka 76 iliyopita na kukataa kuondoka katika ardhi ya mababu zao, hawatairuhusu Marekani na utawala wa Kizayuni kuharibu utambulisho wao wa kitaifa na kihistoria kwa kutumia mbinu nyinginezo."

Baqaei amesema: Mpango wa kusafisha Gaza na kuwahamishia watu wa Palestina katika nchi jirani ni mwendelezo wa mpango wa utawala wa Kizayuni wa wa Israel wa kuwaangamiza kabisa watu wa Palestina, na unapingwa kikamilifu na kulaaniwa kutokana na kupingana kwake waziwazi na misingi na kanuni za sheria za kimataifa na haki za binadamu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria upinzani mkali wa nchi za Kiislamu na kieneo dhidi ya pendekezo la Rais wa Marekani la kuwahamisha kwa nguvu watu wa Gaza na kuwapelekwa katika mchi nyingine kama Misri na Jordan na kisha eneo hilo litwaliwe na Marekani na amesisitiza ulazima wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuwa na msimamo wa wazi na wenye mshikamano katika suala hili.