Baqaei: Marekani imezilenga taasisi za kimataifa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Uraibu wa Marekani wa kutumia sheria nje ya mipaka yake, sasa umezilenga taasisi za kimataifa.
Ismail Baqaei amandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kuhusu matokeo ya kurefushwa vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya taasisi za kimataifa khususan ( Mahakama ya Kimataifa ya Jinai) kitendo ambacho ni sawa na kushiriki katika jinai za Israel kwamba: Uraibu wa Marekani wa kutumia sheria za ndani nje ya mipaka yake sasa umezilenga taasisi za kimataifa.
Baqaei ameeleza kuwa: Kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kutokana na mahakama hiyo kufuatilia na kusikiliza jinai za kutisha za Israel ni fedheha isiyo na kifani katika historia ndefu ya ushirikiano wa Marekani na utawala ghasibu na wa kibaguzi ambao umefanya kila aina ya jinai kwa lengo la "kuiangamiza kikoloni" Palestina.
Amesema, vikwazo dhidi ya Mahakama ya The Hague ni mfano halisi wa matumizi mabaya ya madaraka kwa lengo la kutoa kinga kamili kwa Israel na kuipatia kibali cha kufanya jinai zaidi na hivyo kutishia amani na usalama wa kimataifa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje amesisitiza kuwa: Jamii ya kimataifa inapasa kutambua hatari hii na kuchukua hatua madhubuti.