Pezeshkian: Siasa za Trump kuhusu mazungumzo ni za nyuso mbili
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i122670-pezeshkian_siasa_za_trump_kuhusu_mazungumzo_ni_za_nyuso_mbili
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa sera za rais wa Marekani, Donald Trump dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kusema: "Akiwa juu ya jukwaa (Trump) anasema anataka kufanya mazungumzo na sisi, lakini wakati huo huo anafunga njia zote."
(last modified 2025-02-12T23:23:42+00:00 )
Feb 12, 2025 23:23 UTC
  • Pezeshkian: Siasa za Trump kuhusu mazungumzo ni za nyuso mbili

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa sera za rais wa Marekani, Donald Trump dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kusema: "Akiwa juu ya jukwaa (Trump) anasema anataka kufanya mazungumzo na sisi, lakini wakati huo huo anafunga njia zote."

Rais Masoud Pezzekian alisema hayo jana Jumatano mbele ya mjumuiko mkubwa wa wananchi wa matabaka mbalimbali wa Bushehr, kusini mwa Iran na kuongeza kuwa: Trump anatoa vitisho kwa nchi za dunia nzima kwamba zisiwe na uhusiano wala mazungumzo na Iran lakini wakati huo huo anadai anataka mazungumzo na sisi, kama kweli wewe ni mtu wa mazungumzo, kwa nini unafanya mambo haya?

Rais Pezeshkian pia amegusia jinsi maadui wanavyofanya njama kubwa za kuleta mifarakano ndani ya Iran na kusisitiza kuwa: "Wanaodai kupigania haki za binadamu na amani na utulivu wanatutuhumu kwa uwongo kuwa sisi ni magaidi, lakini wao wenyewe wanafanya mauaji ya kutisha, wameua kigaidi watu 18,000 nchini Iran."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, maadui wa Iran waliingia vitani dhidi ya wananchi wa taifa hili tangu siku za mwanzo kabisa za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa, yule ambaye leo anajifanya kuzungumzia haki za binadamu, amani na utulivu, anaupa silaha utawala wa Israel ili ushambulie kwa mabomu na kuua watu wasio na hatia, na kisha anadai kuwa anapigania amani katika eneo hili.

Amesisitiza kwamba, Iran haitotetereka mbele ya vitisho vyovyote na kusema: "Hatutaki vita na nchi yoyote, tumeanzisha urafiki na majirani zetu wote, majirani zetu wote ni kaka, dada zetu na marafiki zetu, wote ni Waislamu na lazima tuwe na uhusiano wa karibu nao."